OR-TAMISEMI
Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume, amezitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha zinapima maeneo yaliyojengwa vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata hati miliki za maeneo hayo.
Dkt. Mfaume ameyasema hayo alipokuwa katika ziara yake ya ukaguzi wa huduma za afya, lishe na ustawi wa jamii katika mkoa wa Dar es salaam, ambapo alitembelea katika kituo cha afya cha Toangoma kilichopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Temeke
“Ni lazima tupime maeneo yetu, tuweke mipaka rasmi na kuhakikisha yanakuwa na hati miliki ili kuzuia uvamizi kutoka kwa wananchi na kuimarisha utoaji wa huduma za afya,” amesema Dkt. Mfaume
Amesema vituo vingi vya kutolea huduma za afya baadhi ya maeneo ni ya muda mrefu hivyo hakuna sababu ya msingi inayopelekea vituo hivyo kutopimwa na kuwa na umiliki wa hati.
Aidha, Dkt. Mfaume amewataka Waganga Wafawidhi wa vituo vya afya na kamati za usimamizi wa vituo vya kutolea huduma za afya kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa Dini kwani wao ndio mara nyingi huwa karibu na wananchi.
“Hatuwezi kuchora mstari kati yetu sisi wataalam na viongozi katika maeneo yetu, hasa tunapoelekea katika utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote lazima tuungane na viongozi hawa ili kufikisha elimu kwa wananchi” amesisitiza.