Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Daniel Francisco Chapo wakati wa utiaji saini Mikataba na Hati za Makubaliano Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 08 Mei, 2025.
………….
Tanzania na Msumbiji Kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi (JEC) Kuimarisha Ushirikiano wa Biashara na Uwekezaji
Katika hatua ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kushughulikia changamoto za kibiashara kati ya nchi zao, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo, wamekubaliana kuanzisha Tume ya Pamoja ya Uchumi (Joint Economic Commission – JEC).
Makubaliano hayo yamefikiwa leo Mei 8, 2025, wakati wa mazungumzo rasmi yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kitaifa ya siku tatu ya Rais Chapo nchini Tanzania.
Kupitia JEC, Tanzania na Msumbiji zitashughulikia kwa pamoja changamoto za kiuchumi, kuratibu sera na hatua za pamoja za maendeleo, pamoja na kuweka msukumo mpya katika kukuza biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo.
Aidha, marais hao wameafikiana kuboresha mazingira ya biashara na kuwawezesha wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia mifumo rahisi ya biashara (Simplified Trade Regimes – STRs), ili kuchochea shughuli za kiuchumi mipakani na kukuza ajira kwa wananchi wa pande zote mbili.
Kwa kutambua kuwa sekta ya kilimo ndiyo mhimili wa uchumi wa mataifa yao, Tanzania na Msumbiji zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika kilimo, hasa katika zao la korosho, kwa kufanya tafiti za pamoja, kubadilishana maarifa, na kuanzisha umoja wa nchi zinazozalisha korosho na kuuza korosho zilizochakatwa ili kuongeza thamani ya zao hilo katika soko la dunia.
Katika mazungumzo hayo, Rais Dkt. Samia na Rais Chapo pia wamekubaliana kushirikiana katika sekta ya gesi, uchumi wa buluu na rasilimali za baharini ikiwemo uvuvi, madini, utalii na usafirishaji. Ushirikiano huo utahusisha pia kubadilishana uzoefu katika uvuvi wa bahari kuu na kusimamia endelevu rasilimali hizo.
Viongozi hao wamegusia pia umuhimu wa kulinda usalama wa maeneo ya mipaka na kupambana na uhalifu wa kuvuka mipaka, kwa kuimarisha ushirikiano wa kijeshi na kiusalama kati ya nchi hizo.
Akihitimisha mazungumzo yao, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alimpongeza Rais Chapo kwa juhudi zake za kuimarisha umoja wa kitaifa na kurejesha amani na utulivu nchini Msumbiji, akisema kuwa mafanikio hayo yanatoa fursa kwa wananchi wa nchi hiyo kufaidika na matunda ya maendeleo na ushirikiano wa kikanda
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Daniel Francisco Chapo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akisalimiana na Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa kwenye dhifa ya chakula cha mchana aliyoandaliwa Ikulu Jijini Dar es Salaam tarehe 08 Mei, 2025.