Timu ya Simba SC imeibuka na ushindi wa mabao 5-1 dhidi ya Pamba Jiji FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Nyota wa mchezo wa leo ni kiungo Muivory Coast, Jean Charles Ahoua aliyefunga mabao matatu peke yake la kwanza kwa penalti dakika ya 16 na mengine dakika ya 37 na 48, wakati mabao mengine mawili yamefumgwa na mshambuliaji Mcameroon, Christian Leonel Ateba Mbida dakika ya 80 na 84.
Bao pekee la na la kufutia machozi la Pamba Jiji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu limefungwa na mshambuliaji wake tegemeo, Mkenya, Mathew Tegisi Momanyi dakika ya 86.
Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 66 katika mchezo wa 25, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi nne na mabingwa watetezi, Yanga ambao pia wamecheza mechi moja zaidi.
Kwa upande wao Pamba Jiji FC baada ya kupoteza mchezo wa leo wanabaki na pointi zao 27 za mechi 27 sasa nafasi ya 13. Ligi Kuu inashirikisha timu 16 na mwisho wa msimu mbili zitashuka Daraja na mbili nyingine zitakazomaliza nafasi ya 14 na 13 zitamenyana baina yao na mshindi wa jumla atasalia Ligi Kuu.
Timu itakayofungwa itakwenda kumenyana na timu ya Championship kujaribu tena kubaki Ligi Kuu na hadi sasa Ken Gold iliyopanda pamoja na Pamba msimu huu tayari imekwishashuka daraja.