Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Balozi Stephen P. Mbundi leo tarehe 8 Mei, 2025 ameongoza ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kinachofanyika jijini Arusha.
Kikao hicho na kikao cha maafisa waandamizi wa EAC kilichofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 7 Mei, 2025 sehemu ya maandalizi ya Mkutano wa 25 wa Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo utakaofanyika tarehe 9 Mei, 2025.
Kikao hicho cha Makatibu Wakuu kinaangazia vipaumbele vya sekta ya afya katika Jumuiya ikiwemo: Maboresho ya mifumo ya afya inayosomana, ushirikiano katika uchunguzi wa magonjwa ya milipuko na ya kuambukiza, upatikanaji wa teknolojia ya kisasa na bora katika huduma za afya na uimarishaji wa mfumo wa usimamizi wa sekta ya afya.
Akitoa salamu za Serikali katika ufunguzi wa kikao hicho Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia anayeshughulikia masuala ya sayansi, Prof. Daniel Mushi kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi ameipongeza Sekretarieti pamoja na maafisa waandamizi kwa uratibu na maandalizi mazuri ya nyaraka ili kuwezesha Baraza la Mawaziri kutoka na miongozo mizuri ya kisera na kupata uelewa wa pamoja juu ya masuala ya kitaalamu katika masuala ya afya
‘’ Nina imani kuwa majadiliano haya yatatoa uelekeo kwa nchi wanachama katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto za sekta ya afya zilizopo na zinazoendelea kujitokeza ulimwenguni ili kujenga utayari wa pamoja wa kukabiliana nazo’’ Prof. Mushi.
Kadhalika, ameainisha jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutatua changamoto za afya ambazo ni: Kuendelea kuimarisha mfumo wa afya katika pande zake mbili za muungano (Tanzania Bara na Zanzibar) kwa kuboresha miundombinu; uwekezaji wa rasimali watu pamoja na kuwajengea uwezo.
Jitihada nyingine ni pamoja na matumizi ya vifaa tiba vya kidigitali na msisitizo wa ujumuishi na usawa wa upatikanaji wa huduma bora za afya kwa jamii zenye uwezo mdogo na zilizo mbali na huduma za afya.
Viongozi wengine walioshiriki mkutano huu ni pamoja na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Maghembe, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Benjamini Mkapa-Dodoma Prof. Abel Makubi na maafisa wengine waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.