Tume ya Ushindani (FCC) imesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi ili kudhibiti usafirishaji na uingizwaji wa bidhaa bandia kupitia Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni hatua ya kulinda soko la ndani na taswira ya biashara ya kimataifa ya Tanzania.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa semina kwa wadau wa usafirishaji wa bidhaa, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, alisema semina hiyo inalenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu jukumu la kila mdau katika mapambano dhidi ya bidhaa bandia.
“Tunatambua kuwa suala hili haliwezi kushughulikiwa na taasisi moja pekee. Tunahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wadau kama TATOA, TPSF, TNBC, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Uchukuzi na TPA,” alisema Erio.
Aliongeza kuwa FCC inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kuhakikisha ushindani wa haki, ulinzi wa mlaji na udhibiti wa bidhaa haramu, ili kulinda masoko na kuongeza imani ya wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.
Katika mazungumzo hayo, wadau walielezwa kuwa lengo ni kuhakikisha bidhaa zinazopita au kuingizwa nchini zinakidhi viwango vya ubora, huku usafirishaji ukiendelea kwa uaminifu na kwa kuzingatia mikataba ya kibiashara baina ya pande husika.
Erio aliwataka wasafirishaji kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa ili kuepuka migogoro ya kidiplomasia na kuchochea maendeleo ya biashara ya kimataifa kupitia Tanzania.
“Tunapaswa kuhakikisha kuwa Tanzania inabaki kuwa lango salama na lenye kuzingatia viwango vya kimataifa vya biashara,” alisisitiza.