Happy Lazaro,Arusha .
Arusha .Mkuu wa Mkoa wa Arusha, amefungua rasmi Jukwaa la Uwekezaji la Mkoa wa Arusha linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC, akisisitiza umuhimu wa Watanzania hasa wakazi wa Arusha, kuona na kutumia fursa zilizopo ndani ya mkoa huo
Makonda amesema kuwa lengo kuu la jukwaa hilo ni kuwapa wananchi uelewa wa kina kuhusu namna ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali za uchumi zinazokua kwa kasi mkoani humo, akisisitiza kuwa haipaswi tu kuwa wasikilizaji wa mada, bali wachukua hatua.
“Tunategemea viongozi na wataalam waliokuja hapa watuambie tukitoka hapa fedha zinapatikanaje na wananchi wawekeze fedha zao wapi ili wasipate hasara,” amesema Makonda .
Akitoa mfano wa fursa iliyopo sasa, Makonda ametaja mashindano ya AFCON yanayotarajiwa kufanyika katika mkoa wa Arusha, amesema kuwa, Mbali na kushangilia mpira, ni vyema kujua Watanzania watanufaika vipi kiuchumi.
Ameongeza kuwa mkoa wa Arusha ni mkoa wenye neema ya miradi mikubwa ya maendeleo iliyoanzishwa chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, laikini wananchi walio wengi hawawafahamu fursa hizo zinazopatikana kwenye miradi hiyo
“Leo tunataka tuangazie maeneo ambayo tunaweza kubadilisha maisha yetu na ya vijana wa Arusha, Watanzania na hata wageni wanaotamani kushirikiana nasi,” amesisitiza.
Jukwaa hilo linatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kwa wawekezaji, wajasiriamali, na watunga sera kuhusu namna ya kufanikisha maendeleo ya pamoja kupitia uwekezaji wa kimkakati katika sekta zenye tija.