Dar es Salaam
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Skauti Tanzania wamemlalamikia Kamishna wa Skauti, Abubakari Mtitu, kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka, na kumtaka Waziri wa Elimu kuunda tume maalum ya kuchunguza sakata hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkufunzi Msaidizi wa Skauti (ALT), Noel Mavula, alisema kuwa Kamishna huyo anadaiwa kuvunja taratibu na maadili ya chama kwa kushiriki kupanga safari ya kimataifa kwa vijana wasiostahili.
Mavula alieleza kuwa kulikuwepo na tamasha la Skauti la Dunia lililolenga kuwashirikisha vijana kutoka familia masikini ili wapate fursa ya kujifunza nje ya nchi. Hata hivyo, alidai kuwa waliokwenda kwenye tamasha hilo walikuwa ni vijana kutoka familia zenye uwezo mkubwa wa kifedha, kinyume na malengo ya makao makuu ya Skauti duniani.
“Skauti ni chama cha kimaadili. Kitendo cha Kamishna Mkuu kumpeleka mtoto wake kwenye tamasha hilo ni ukiukwaji mkubwa wa maadili na matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Mavula.
Aliongeza kuwa kwa nafasi yake, Waziri wa Elimu ambaye pia ni Rais wa chama hicho, anapaswa kuchukua hatua kwa kuwa mgogoro huu wa kiuongozi ndani ya chama umekuwepo kwa muda mrefu bila kutatuliwa.
“Tunaomba uchunguzi ufanyike na hatua zichukuliwe dhidi ya wote waliohusika, kuanzia Kamishna Mkuu mwenyewe. Kama mtoto wake ndiye alipewa nafasi hiyo, ni dhahiri kuwa kulikuwa na upendeleo,” alisema.
Mavula alisisitiza kuwa wao kama viongozi wa ngazi ya chini ni kama wapiga filimbi, na kazi yao ni kuonyesha pale ambapo maadili yanakiukwa ili mamlaka husika zichukue hatua.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Skauti Tanzania, Abubakari Mtitu, alipoulizwa kuhusu tuhuma hizo kwa njia ya simu, alikanusha madai hayo akisema kuwa hayana ukweli. Alisisitiza kuwa taarifa hizo ni za uongo na zina lengo la kumchafua, huku akitaka mwandishi kufika ofisini kwake kwa mahojiano rasmi ili kupata taarifa sahihi.