TIMU ya Simba SC imetoka nyuma na kushinda mabao 2-1 dhidi ya Mashujaa FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Mabao yote ya Simba SC leo yamefungwa kwa mikwaju ya penalti na mshambuliaji Mcameroon, Christian Leonel Ateba Mbida dakika ya 65 na 90’+19 baada ya mshambuliaji mzawa, Jaffar Salum Kibaya kuanza kuifungia Mashujaa FC dakika ya tano.
Simba walipata bao la pili Mashujaa ikiwa pungufu baada ya kipa wake, Patrick Evans Mumthali kutolewa kwa nyekundu dakika ya 77 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Kiungo Abdulnasir Assa Mohamed ndiye aliyekwenda kusimama langoni kwa sababu Mashujaa ilikuwa imemaliza nafasi za mabadiliko na alikaribia kumalizia vizuri kama si kuruhusu bao la penalti ya dakika ya mwisho.
Kwa ushindi huo, Simba SC imefikisha pointi 60 katika mchezo wa 23, ingawa inabaki nafasi ya pili ikizidiwa pointi 10 na mabingwa watetezi, Yanga ambao pia wamecheza mechi tatu zaidi.
Mashujaa baada ya kupoteza mchezo huo inabaki na pointi zake 30 baada ya kucheza mechi 27 sasa ikibaki nafasi ya tisa.