Timu za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa zimefanikiwa kunyakua vikombe vinne vya michezo ya Mei Mosi Taifa 2025 iliyofanyika mkoani Singida kuanzia tarehe 14 Aprili,2025 na kuhitimishwa tarehe 29 Aprili,2025 katika viwanja vya Liti mkoani Singida.
Vikombe hivyo ni Kikombe cha mshindi wa kwanza Mpira wa Kikapu wanawake, Kikombe cha Mshindi wa Kwanza Vishale (Darts) wanaume, Mshindi wa tatu Mpira wa Pete (Netball) na Mshindi wa tatu vishale (Darts) wanawake.
Akikabidhi vikombe hivyo kwa wanamichezo walioshinda zawadi, Waziri wa Nchi Ofisi wa Waziri Mkuu Kazi Ajira Vijana na wenye Ulemavu, Mheshimiwa Ridhiwan Kikwete (Mb) amewapongeza wafanyakazi kwa kuonyesha ushindani katika michezo mbalimbali iliyoshindaniwa.
Awali Mheshimiwa Kikwete, alishuhudia Fainali ya Mpira wa Miguu kati ya Tanesco na Hazina uliofanyika katika uwanja wa CCM Liti, ambapo Hazina waliibuka na ushindi wa goli 1- 0 lililofungwa katika kipindi cha pili.
Mashindano ya Mei Mosi yaliyoisha tarehe 29, Aprili 2025 itahimishwa na Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi ya Mei Mosi ambayo ni siku ya Wafanyakazi Duniani itakayoadhimishwa tarehe 01 Mei,
2025, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi ambapo pamoja na mambo mengine atawahutubia wafanyakazi pamoja na kutoa zawadi kwa timu zilizofanya vizuri kwenye michezo ya Mei Mosi Taifa 2025.