Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Saidi Mohamed Mtanda amsema kutokana na miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea mkoani hapo, anatarajia vyanzo vipya vya kodi vitazaliwa na kuufanya mkoa Mwanza kuwa na mchango mkubwa zaidi katika uchumi nchi.
Ameyasema hayo leo tarehe 30.04.2025 alipokutana na ujumbe wa Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ukiongozwa na Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Bw. Richard Kayombo walipofika kujitambulisha wakati wa zoezi la Elimu ya Mlipakodi mlango kwa mlango.
Mhe. Mtanda ameeleza kuwa mkoa Mwanza umekuwa miongoni mwa mikoa Minne bora inayochangia kiasi kikubwa katika pato Ghafi la taifa (GDP) kwa asilimia 7.2 ambayo inatokana na ulipaji kodi mzuri kwa walipakodi wa mkoani hapo ambapo mpango ni kufikia mchango wa asilimia 10 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa bandari na ununuzi wa Meli na vivuko na ujenzi wa Daraja la Magufuli.
“Mkoa wetu kwa sababu ya ulipaji mzuri wa kodi unachangia Pato Ghafi la Taifa (GDP) kwa asilimia 7.2 na matarijio yetu kwenda hadi 10 mpaka kufikia 12 baada ya miradi inayochochea uchumi kukamilika kama vile Trani ya umeme (SGR) na Upanuzi wa bandari “
Aidha, Mhe. Mtanda amewashukuru walipakodi wa mwanza kwa kuendelea kulipa kodi kwa hiari na kuwataka kuenedelea kulipa kodi ili kuiwezesha serikali kukamilisha miradi inayoendelea na kuweza kuanzisha mipya.
Pia amewahimiza wafanyabiashara kukahakisha wanatoa risiti kwa kila mauzo wanayoyanfa bila ya kushurutishwa na wananchi nao kudai risiti.
Nae Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipakodi na Mawasiliano Bw. Richard Kayombo amesema lengo la Zoezi la elimu kwa Mlipakodi mlango kwa mlango ni kuweza kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ili kuwafikishia elimu ya kodi sambamba na kusikiliza changamoto zao kwa sababu kuna baadhi ya wafanyabiashara hawahudhurii Semina za kodi hivyo wanaweza kupatikana kwa kuwatembelea katika maeneo yao ya biashara kupitia zoezi hilo.