Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu amemhakikishia Waziri mpya wa usafirishaji wa Comoro Bi. Hassane Alfeine Yasmine kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo katika sekta ya usafirishaji wa Angani na Baharini.
Balozi Yakubu alimueleza Bi Hassane kuwa sekta anayoiongoza ndio kiungo muhimu cha biashara baina ya nchi zao na kutaja mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika sekta tajwa ikiwemo hivi sasa kuwepo kwa usafiri wa ndege baina ya Dar es salaam na Moroni kila siku.
Kwa upande wake,Bi Hassane alipongeza ushirikiano uliopo katika sekta ya usafiri wa anga na majini na kushauri kuwepo kwa majadiliano zaidi ili kuondoa changamoto katika usafiri wa baharini ikiwemo kuboresha maeneo mahsusi ya mizigo ya Comoro katika bandari ya Dar es salaam,ubora wa meli za mizigo baina ya nchi hizo na pia kuongeza ubadilishanaji wa ujuzi kwa mamlaka za viwanja vya ndege.