John Bukuku, Dar es Salaam.
Wahariri wa vyombo vya habari wamekutana jijini Dar es Salaam kushiriki semina maalum kuhusu namna ya kupinga vitendo vya rushwa katika kipindi cha uchaguzi. Semina hiyo imeandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, utakaohusisha uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Wabunge na Madiwani.
Akizungumza wakati wa kufungua semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila, alisema kuwa vyombo vya habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru, wa haki na usiohusisha vitendo vya rushwa.
“Vyombo vya habari vina jukumu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kupinga masuala ya rushwa, hasa tunapoelekea katika kipindi cha uchaguzi,” alisema Chalamila.
Alisisitiza kuwa ni muhimu elimu hiyo ifikie kila mpiga kura, jambo ambalo haliwezi kufanikishwa bila kushirikiana na vyombo vya habari. Alieleza kuwa vyombo hivyo vina nafasi ya kuelimisha jamii juu ya athari za kutoa na kupokea rushwa, pamoja na umuhimu wa kuchagua viongozi kwa misingi ya sera zao, si kwa rushwa.
“Warsha hii itawawezesha wahariri kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa kuwapa elimu ya kupinga rushwa, jambo litakalosaidia kuhimiza uwajibikaji kwa viongozi,” aliongeza.
Chalamila alisema vitendo vya rushwa vinaharibu misingi ya kidemokrasia na utawala bora kwa kutoa upendeleo kwa wagombea wanaotoa rushwa na kuwanyima nafasi wale wasiohusika na vitendo hivyo. Hali hii, alisema, husababisha kuchaguliwa kwa viongozi wala rushwa, jambo ambalo linawavunja moyo wananchi na kupunguza imani yao kwa mifumo ya utawala na taasisi za serikali.
“Rushwa hudhalilisha utu na thamani ya mtu. Ili kuzuia hali hii, kuna hatua nne muhimu ambazo ni kuhakikisha uteuzi wa wagombea unazingatia usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo,” alifafanua.
Aliongeza kuwa ni lazima kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za umma, fedha za kampeni, na kuhakikisha vyama vyote vya siasa na wagombea wanapata fursa sawa. Aidha, mazingira ya upigaji kura yanapaswa kuwa salama na ya haki, bila vitisho au upendeleo, na malalamiko kushughulikiwa kwa uwazi na haki.
Chalamila alibainisha kuwa serikali tayari imeanza kuchukua hatua kadhaa ili kuhakikisha uchaguzi wa 2025 unakuwa huru na wa haki. Alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada zake za kupambana na rushwa.
“Namshukuru sana Rais Samia kwa namna anavyopambana na masuala ya rushwa ili kuimarisha mapambano dhidi ya janga hili,” alihitimisha.