Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Wilson Mahera akizungumza wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa shule na Walimu kuhusu matumizi bora na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yaliyoandaliwa kwa udhamini wa mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) katika hafla iliyofanyika leo Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.
Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali kutoka TAMISEMI, Bi. Suzanne Nusu akizungumza wakati kufunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa shule na Walimu kuhusu matumizi bora na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yaliyoandaliwa kwa udhamini wa mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) katika hafla iliyofanyika leo Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.
Washiriki wa mafunzo ya matumizi bora na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wakiwa katika hafla ya kufunga mafunzo hayo yaliyoandaliwa kwa udhamini wa mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) iliyofanyika leo Aprili 29, 2025 katika ukumbi wa Shirika la Elimu Kibaha mkoani Pwani.
…..
NA NOEL RUKANUGA, PWANI
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Wilson Mahera, amewataka viongozi wanaosimamia sekta ya elimu kuanzia ngazi ya Mkoa hadi shule kuimarisha usimamizi wa ufundishaji na ujifunzaji, huku akisisitiza umuhimu wa walimu kuongeza bidii na ubunifu katika kutatua changamoto zinazoikabili sekta hiyo muhimu nchini.
Dkt. Mahera ametoa maagizo hayo leo Aprili 29, 2025 Kibaha Mkoani Pwani, wakati akifunga mafunzo ya kuwajengea uwezo Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule na Walimu kuhusu matumizi bora na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), yaliyoandaliwa kwa udhamini wa mradi wa Boost.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Dkt. Mahera amesema kuwa usimamizi makini wa walimu ni kichocheo kikubwa cha uboreshaji wa elimu, kwani ni jukumu la kila mmoja kutumia maarifa na rasilimali zilizopo kuwapa wanafunzi elimu bora itakayowawezesha kujiajiri au kuajiriwa.
Dkt. Mahera amesema jumla ya washiriki 1,800 wakiwemo Maafisa Elimu Kata 600, Walimu Wakuu 600, na Walimu wa TEHAMA 600 kutoka Halmashauri zote 184 wamepatiwa mafunzo hayo kwa lengo la kuongeza ufanisi katika kufundisha na kujifunza kwa kutumia TEHAMA.
“Nawapongeza washiriki wote kwa kupata mafunzo ya TEHAMA kupitia mradi wa Boost. Tuna imani kuwa mkiondoka hapa mtakwenda kutekeleza mliyoyajifunza kwa vitendo,” amesema Dkt. Mahera.
Amesisitiza kuwa vifaa vya TEHAMA vitakavyotolewa shuleni ni mali ya umma na vinapaswa kutunzwa kwa uangalifu mkubwa, huku akionya dhidi ya matumizi yasiyo sahihi ya vifaa hivyo na kuwataka wakuu wa shule kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika kwa lengo lililokusudiwa.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mahera amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutenga bajeti maalum kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya vituo vya walimu, ili kuwezesha mafunzo endelevu ya kila mwezi yanayolenga kukuza taaluma na mbinu za kisasa za ufundishaji.
Ameongeza kuwa serikali itaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa walimu kama sehemu ya kuimarisha elimu nchini, huku akihimiza kuwepo kwa mikakati ya kuwalinda wanafunzi dhidi ya ukatili, hasa wa kijinsia.
Amesisitiza kuwa jukumu la kuwalinda watoto ni la kila mwalimu, na ni sehemu ya kuhakikisha taifa linakuwa na kizazi salama na chenye maadili.
Aidha, ametoa wito kwa kila mkoa na halmashauri kuhakikisha shule zote za kutwa zinatoa huduma ya chakula kwa wanafunzi ili kuongeza usikivu na tija katika masomo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Awali kutoka TAMISEMI, Bi. Suzanne Nusu, ameeleza kuwa mafunzo hayo ya TEHAMA ni muhimu sana kwani yanawawezesha walimu na wakuu wa shule kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Washiriki wa mafunzo hayo wametoa shukrani kwa serikali kupitia mradi wa Boost kwa kutoa mafunzo yenye tija na yaliyolenga kuinua kiwango cha elimu nchini.
Afisa Elimu wa Kata ya Murusagamba, Wilaya ya Ngara Mkoani Kagera, Bi. Catherin Herintee, ameiomba serikali kuongeza muda wa mafunzo kama hayo ili kuwapa walimu uelewa wa kina kuhusu TEHAMA na kuwafikia walimu wengi zaidi katika maeneo mbalimbali hasa vijijini.