Na WAF – Tabora
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema zoezi la madaktari bingwa kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa wananchi ni endelevu kwani Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuendelea na kuingizwa kwenye mipango ya afya nchini.
Waziri Mhagama amesema hayo wakati akizindua awamu ya tano ya zoezi la Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi mkoani Tabora Aprili 28,2025, ambapo zoezi hilo linatekelezwa nchi nzima kwa kipindi cha miezi miwili kuanzia April 28 hadi Juni 28 2025.
“Zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa katika awamu zilizotangulia kwa kuwafikia wananchi 154, 015 lakini pia kuwajengea uwezo wataalam wa afya wapatao 9,434, Mhe. Rais ameona ipo haja ya program hii kuwa endelevu na kuingizwa kwenye mipango ya wizara ya Afya,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama ameongeza kuwa, watu wengi walikuwa wanashindwa kupata huduma za kibingwa kutokana na upatikanaji wake, lakini kutokana na maono ya Rais Samia leo huduma zimesogezwa kwa wananchi.
Awali akielezea lengo la Programu hiyo ya Madaktari Bingwa wa Rais Samia Dkt. Ahamad Makuwani amesema, mwanzo walilenga kuwajengea uwezo wataalam ngazi za msingi, lakini baada ya kuona mafanikio ndio ukawa mwanzo wa kutanua wigo wa zoezi na kuwa huduma.
Akitoa salaam za mkoa, Kaimu Mkuu wa mkoa wa Tabora Mhe. Deusdedit Kitwale, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora mjini, amesema wamefanya uhamasishaji wa kutosha huku akiwataka wananchi kujitokeza kwenda kupima afya zao na wakibainika kuwa na changamoto za afya wapatiwe matibabu.
“Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutuheshimisha kwa kutusogezea huduma karibu na wananchi, hivyo ni rai yangu sisi wananchi wa Tabora tulione hili na tujitokeze kwa wingi siku zote sita,” amesema Mhe. Kitwale.
Naye Mwakilishi wa Madaktari Bingwa Dkt. Mike Mabimbi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa Mwanza Sekoutoure, akitoa uzoefu walioupata kwenye zoezi lililotangulia, amesema watu wengi walikuwa na matatizo lakini walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya uchumi na kushindwa kuwafikia mabingwa, hivyo kitendo cha wao kufanya kambi hizo imekuwa ukombozi kwao.
Mkoa wa Tabora umepokea jumla ya Madakatari Bingwa na Bingwa Bobezi 64 watakaotoa huduma za kibingwa kwenye halmashauri zote nane(8) za mkoa huo kwa siku sita kuanzia April 28 hadi Mei 03 2025.