Spika wa Bunge la Comoro,Moustadroine Abdou amesifu ushirikiano mzuri wa Tanzania na Comoro.Spika Moustadrione ameyasema hayo katika hafla ya chakula cha jioni kuadhimisha miaka 61 ya Muungano iliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Spika Moustadrione amezungumzia pia uhusiano mzuri uliopo baina ya Marais Azali Assoumani na Samia Suluhu Hassan ambapo ameeleza pia namna Comoro na Tanzania zilivyo na fursa nzuri ya ushirikiano wa faida.
Spika Moustadroine pia alipongeza maendeleo ambayo Tanzania imepiga kwa kutoa ushuhuda wake wa ziara aliyofanya hivi karibuni ambapo maeneo yote aliyotembelea ikiwemo Hospitali ya Benjamin Mkapa,Chuo Kikuu cha Dodoma,Reli ya SGR na mengineyo hatua hizo ni somo zuri kwa nchi za Afrika.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu alieleza kuwa Sherehe za miaka 61 ni kipimo kizuri cha ushirikiano wa nchi hizo ambapo ushirikiano umekuwa zaidi katika kipindi cha mwaka mmoja kutokana na mawasiliano ya karibu ya Marais Samia Suluhu Hassan na Azali Assoumani jambo linalomrahisishia kazi na tangu amefika tayari mikataba mingi ya ushirikiano imesainiwa na mingi zaidi iko katika hatua ya majadiliano kabla ya kusainiwa.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na Mawaziri takriban saba ikiwemo wa Nishati,Jinsia,Habari,Sheria,Usafirishaji,Ulinzi,Mambo ya Ndani na viongozi waandamizi wakiwemo wasaidizi wa Rais wa nchi hiyo,Mkuu wa Majeshi,Wakuu wa Taasisi za Umma,Mabalozi wanaowakilisha nchi zao na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa.
Sherehe hizo zilipambwa na vikundi vya burudani toka Tanzania na Comoro.