Daktari bingwa wa magonjwa yatokanayo na kazi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group Elias Birago akitoa ushauri wa afya ya moyo kwa Nelson Mnyanyi aliyetembelea banda la taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Mandewa, mkoani Singida.
Afisa Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Makrina Komba akimpima urefu na uzito mkazi wa Singida aliyefika katika Maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali Pa Kazi yanayofanyika katika viwanja vya maonesho Mandewa mkoani Singida.
……….
Na Jeremiah Ombelo – Singida
26/04/2025 Katika jitihada za kuboresha huduma za afya nchini, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa huduma za uchunguzi na elimu kwa wananchi kuhusu njia bora za kujikinga na magonjwa ya moyo kupitia maonesho ya Kimataifa ya Wiki ya Usamala na Afya Mahali pa Kazi.
Uchunguzi na elimu hiyo vinafanywa na Taasisi hiyo katika viwanja vya maonesho vya Mandewa vilivyopo mkoani Singida.
Taasisi hiyo inatoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo kwa kutumia mashine za kisasa zinazoweza kugundua tatizo la mgonjwa mapema pamoja na kutoa ushauri wa kitaalamu kutoka kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo.
Huduma hizo zimekuwa zikitolewa bila gharama kama sehemu ya kuihamasisha jamii kuwa na tabia ya kuchunguza afya lakini pia kama sehemu ya kuhamasisha afya bora mahali pa kazi.
Aidha wananchi wanaopatikana na viashiria vya magonjwa ya moyo wanapewa ushauri wa kitaalamu na wengine kupewa rufaa kwaajili ya matibabu zaidi.
Maonesho hayo yamekuwa fursa kwa wakazi wa mkoa wa Singida na mikoa ya jirani kupata huduma za uchunguzi wa magonjwa ya moyo na kuongeza uelewa wao kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa hayo.