Washiriki zaidi ya 100 wa Jukwaa la Pili la Utalii wa Vyakula kutoka nchi mbalimbali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Nkoba Mabula jana Aprili 25, 2015 wamefanya ziara ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Arusha kujionea vivutio vya utalii ambavyo vinapatikana ndani ya hifadhi hiyo.
Washiriki hao walipokelewa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kaskazini pamoja na menejimenti ya Hifadhi ya Taifa Arusha na kupata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya kuvutia ndani ya hifadhi, yakiwemo maziwa ya asili, maporomoko ya maji, sehemu za miinuko zenye mandhari ya kuvutia sambamba na kushuhudia makundi makubwa ya wanyamapori wakiwemo Pundamilia, Twiga, Nyati na wanyama wengine wengi wa kuvutia.
Ziara hiyo ya washiriki wa Jukwaa la Pili la Utalii wa Chakula ndani ya Hifadhi ya Taifa Arusha ni kufuatia kumalizika kwa Jukwaa la Pili la Utalii la Vyakula vya Asili ambalo liliandaliwa na shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kwa kanda ya Afrika ambapo mkutano wake ulifanyika kuanzia tarehe 23 Aprili 2025 katika Hoteli ya Gran Melia iliyopo jijini Arusha na kuhitimishwa leo Aprili 25, 2025.