Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Katika kuadhimisha miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Wilaya ya Same imefanya tukio maalum la upandaji wa miti 500 katika Shule ya Sekondari Same. Tukio hilo limeambatana na wito wa kuendeleza amani, mshikamano, na kulinda mazingira kwa ustawi wa sasa na vizazi vijavyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Bi. Upendo Wella, aliwataka wananchi kuuenzi Muungano kwa kudumisha amani, upendo, mshikamano na kutunza mazingira. Alisisitiza kuwa juhudi hizi si tu husaidia maisha yetu ya sasa, bali pia zinaweka msingi bora kwa vizazi vijavyo.
Pia, Bi. Wella alieleza kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka kipaumbele kikubwa katika masuala ya uhifadhi wa mazingira huku akisisitiza kuwa taasisi za elimu zina jukumu kubwa la kulea kizazi chenye uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira, na akahimiza kila mwananchi kushiriki kikamilifu kwa kupanda na kutunza miti.
Kwa upande wake, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi kutoka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Kaskazini, Bw. James Samweli, alisema jumla ya miti 500 imepandwa kama sehemu ya maadhimisho hayo. Alibainisha kuwa TFS itaendelea kutoa miche bure kwa wananchi na taasisi mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha kila mmoja anakuwa balozi wa mazingira.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bw. Jimson Mhagama, alisema kuwa Halmashauri na taasisi zake zitaendelea kusimamia kikamilifu jitihada za upandaji miti, hasa katika msimu huu wa mvua, ili kuimarisha jitihada za kuhifadhi mazingira.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika rasmi tarehe 26 Aprili 1964. Mwaka huu, Watanzania wanaadhimisha miaka 61 ya Muungano huo muhimu, ambao unaendelea kuwa msingi wa mshikamano, amani na maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.