Na Mwandishi wetu – Singida
Timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inayocheza Mpira wa Kikapu ya wanawake imeichezesha kwata timu ya mpira wa Kikapu ya Ikulu baada ya kuichapa bila huruma seti 73 kwa 42 katika mchezo mkali uliopigwa katika uwanja wa Shule ya Msingi Mwaja nje kidogo ya mji wa Singida.
Michezo ulianza kwa timu zote zikisomana kwa kila upande na huku zikishambuliana kwa zamu lakini ndiyo Ulinzi ndiyo walikuwa wa kwanza kulisakama goli la Ikulu kila wakati na hatimaye wakafanikiwa kutangulia kwa tofauti ya seti 10 ambazo Ikulu kwao hawakuweza kuzifuta.
Mara baada ya mchezo makocha wa pande zote mbili walipohojiwa walionesha kukubaliana na matokeo ya mchezo, ambapo kwa upande wa Ulinzi kocha Bi. Lulu Joseph alijinasibu kuwa ubora wa timu yake ndiyo uliombeba mpaka kupekea apate matokeo hayo.
Kwa upande wake Kocha wa Ikulu Bw. Haleluya Kavalambi alikiri kuzidiwa ubora na Ulinzi na kusema kuwa zipambanapo timu mbili lazima mmoja mwisho wa siku aibuke kuwa mshindi.
Naye Mwenyekiti wa Ulinzi Sports Club Bw. Malcus Nyanda amewapongeza wachezaji wote pamoja na benchi la ufundi kwakupambana mwanzo wa mchezo hadi mwisho walipojihakikishia kuwa wametwaa ubingwa huo wa kihistoria.
Wakati huo huo katika mchezo wa kwanza wa kutafuta mshindi wa tatu wa mchezo wa Kikapu Wanawake timu ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeshika nafasi ya tatu baada ya kuichapa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Seti 72 kwa 60.
Fainali ya mpira wa Kikapu katika michezo ya Mei Mosi mwaka huu ndiyo inafanyika kwa mara ya kwanza baada ya mchezo huo kuongezewa katika orodha ya michezo inayoshindaniwa, hivyo bingwa wa mchezo huo ambaye ni Ulinzi atakuwa bingwa wa kwanza wa Kihistoria kwa kulitwaa kombe hili kwa mara ya kwanza.