Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amemwelekeza Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga kupitia ofisi ya Kamishna wa ardhi nchini kuunda timu kushughulikia mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Kitongoji cha Luhafwe na hamashauri ya Tanganyika mkoani Katavi ndani ya wiki tatu.
Waziri Ndejembi ameitaka timu ya wizara itakayokwenda kutatua mgogoro huo, kupitia historia yote ya eneo hilo la Kitongoji cha Luhafwe na kuwasisitiza wananchi hao kuwa na amani na utulivu wakati mgogoro huo unafanyiwa kazi.
“Kaya zilizofanyiwa sensa zibaki kuwa hizi zisiongezeke, kwa sababu kadri mnavyoongeza kaya ndipo mnapoleta ugumu wa kutatua mgogoro huu. Msitishe uuzaji wowote wa ardhi unaotokana na mwananchi na mwananchi mpka hapo tutakapopata suluhu ya mgogoro huu” amesema Waziri Ndejembi.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananachi wa Kitongoji cha Luhafwe Kijiji cha Vikonge kata ya Tongwe mkoani Katavi Aprili 23, 2025, Waziri wa Ardhi, amesema serikali haitaki kumwonea mtu kwenye haki yake na kusisitiza kuwa wizara yake itapeleka timu ambayo itashirikiana na timu ya mkoa na wananchi ili kupata suluhu ya kudumu kuhusu mgogoro wa ardhi katika Kitongoji cha Luhafwe mkoani humo.
“Serikali inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haitaki kumwonea mtu yoyote na wala haina nia ya kumwonea mtu kwenye haki yake” amesema
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe. Mwanavua Mrindoko amesema ofisi yake itashirikiana na timu hiyo na kuwasihi wananchi wa kuwa watulivu wakati suala hilo linafanyiwa kazi.