Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Dunia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi kupitia misaada, mikopo nafuu na utaalamu wa kiufundi ambao Taasisi hiyo kubwa ya Fedha Dunia inaipatia Tanzzania kwa miongo kadhaa sasa.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, Makao Makuu ya Benki hiyo Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Pamoja na kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha zinazotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, Dkt. Nchemba alionesha furaha yake kwa Benki ya Dunia kuonesha utayari wake wa kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa kimkakati wa Reli ya Kisasa (SGR).
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba alimkumbusha Dkt. Kibwe, kuhusu maombi ya Tanzania ya kutaka Kiswahili kiwe sehemu ya lugha rasmi za mawasiliano katika mikutano ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia kutokana na umuhimu wake katika maendeleo ya Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla.
Katika kikao hicho pia alishiriki Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, aliyezungumzia kuhusu kuanza kwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 itakayosaidia kuchochea maendeleo ya watu na kukuza uchumi wa nchi, huku Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, aliyeshukuru kwa mchango wa Benki ya Dunia katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya Zanzibar.
Uwekezaji wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania umefikia dola za Marekani bilioni 10.9 ambapo miradi 38 ya maendeleo inatekelezwa katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, maji, elimu, nishati, ujenzi wa miundombinu ya Barabara, na huduma za kijamii ikiwemo masoko na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia, anayesimamia Kundi la Kwanza la nchi za Kanda ya Afrika (Africa Group 1 Constituency), ambaye ni Mtanzania, Dkt. Zarau Wendeline Kibwe, alisema Benki ya Dunia inathamini ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Benki yake na Tanzania.
Alibainisha kuwa Benki ya Dunia itaendeleza ushirikiano huo kupitia mwelekeo mpya wa kisera ambapo msisitizo mkubwa umewekwa katika maeneo matano yenye kuziwezesha nchi wanachama hususan zilizoko katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuwekeza kwenye miradi itakayochangia kukuza ajira, kupitia sekta za kilimo biashara, ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli, nishati, afya, utalii na uzalishaji viwandani vitakavyo changia kuongeza thamani ya bidhaa.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dkt. Elsie Kanza, Kamishna Msaidizi wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Robert Mtengule, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha, Bi. Zawadi Maginga na Viongozi wengine kutoka Wizara ya Fedha na Benki ya Dunia.





