


Na Mwandishi Wetu,Dodoma
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira amemjia juu Mwanasheria maarufu na mwanasiasa wa nchini Kenya Martha Karua, ambaye amekuja nchini kumtetea Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu, anayekabiliwa na tuhuma za uhaini na kuchapisha picha za uongo mtandaoni.
Wasira amemtaka mwanasheria huyo kuacha kujipima uzito na Chama Cha Mapinduzi huku akimwambia pia kuwa Chama kinaheshimu mamlaka ya Mahakama na Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).
Amesisitiza kama Karua anajiona anaweza kushughulika na migoro basi atatue matatizo yaliyoko nchini kwake au mgogoro unaoendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Akizungumza mbele ya wananchi wa Mkoa wa Dodoma jana, akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuelezea faida za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Wasira alitumia nafasi hiyo kumjibu Karua hatua kwa hatua na kumtaka aache kuingilia mambo asiyoyajua vizuri.
“Tanzania hatuvurugi amani ya Afrika Mashariki isipokuwa tunaendesha mambo yetu kwa amani na salamu ninazompatia Mwanasheria Martha Karua ni kwamba aache kujipima na CCM, CCM ni chama kikubwa Afrika kinachoanza na nyumba kumi,” alisema.
Aliongeza kuwa “CCM haina hofu na chama chochote lakini hatuwezi kuingilia kazi ya Mahakama na hatuwezi kuingilia shughuli za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwa ni vyombo vyenye mamlaka, lakini kama ni mjuzi ashughulike na mambo ya Kenya.”
Kulingana na Wasira aliyekuwa akizungumza hayo huku akishangiliwa na umma, alisema kama anaona chama chake ni kidogo na anataka umaarufu basi aangalie mataifa mengine ya Afrika yenye migogoro akatatue.
“Akishindwa arudi nyumbani akaendeshe chama chake ambacho sera zake hazijulikani. Atuache Tanzania tuchaguane kwa utaratibu wetu hata mwenyewe na zungumza hapa nilichaguliwa kwa kishindo katika nafasi hii ndani ya Chama, naamini dozi hii inamtosha,” amesema
Alisema katika uchaguzi uliopita Kenya, Martha alikuwa mgombea Mwenza wa Raila Odinga, walikuwa wanalalamikia uamuzi wa tume yao ya uhaguzi walienda hadi ‘Supreme Cort (Mahakama ya juu), lakini hawakupata kitu akaenda Mahakama ya Afrika Mashariki na alitoka patupu.
“Kama alitoka patupu amuache Lissu na kesi yake matokeo yatapatikana na yeye atayakubali kama alivyokuyakubali yale ya Kenya,” alieleza.
Wakati Wasira anamjibu mwanasheria huyo wa Kenya alisema Chama kinamheshimu kwa kuwai ni mtu wa Afrika Mashariki, pia kinaheshimu taaluma yake ya sheria.
Martha ni Mwenyekiti wa Chama cha People’s Liberation Party (PLP) cha Kenya.
“Anahaki kama mwanasheria kama ameitwa na watu wanaoshtakiwa, sasa pale kuna ‘katatizo’ tuna Polisi, Mahakama na Tundu Lissu. Sasa Polisi wakikukuta umekosea hawaendi kwa Wasira kusema kwamba umekosea wao wamesomeshwa kujua kama umekosea, wakikuchukua hawaruhusiwi kukaa na wewe muda mrefu.
“Wanakuambia ukae ikifika saa 24 uwe umeshafika mahakamani kwa sababu kwa mujibu wa katiba, Mahakama ndicho chombo cha kikatiba cha kutoa haki hapa nchini, sasa polisi walimkuta Lissu wakamchukua…
“Lakini hapa duniani imewekwa mahakama ndicho chombo kinachotoa haki, hatuingilii kukiamrisha, na sasa Martha Karua mwanasheria aliebobea anajua mgawanyo wa mamlaka kwamba ukiwa na mahakama Rais hawezi kuingilia mahakama.
“Anajua mahakama peke yake ndiyo inaweza kuamua mtu kakosea au hajakosea na sheria inasema mtu hawezi kuhesabiwa kosa mpaka mahakama imuone ana kosa kwa hiyo hatujui kama anakosa ama laa, polisi ndio wanajua na Mahakama ndio imepelekewa.” alisisitiza.
Akifafanua zaidi Wasira alisema
Lissu angekuwa hana kosa wangemuachia na juzi walimkamata mwingine anaitwa Heche (John Heche ambaye ni Makamu MwenyekitiwaChadema) Bara, lakini wakamshikilia kwa muda wakamuachia.
“Na sisi Chama Cha Mapinduzi na serikali tuliyoiunda kwa idhini ya Watanzania hatuingilii Mahakama, tunaiachia Mahakama ifanye kazi yake hatuiambii imuachie au imfunge Martha Karua anajua hayo mambo lakini kaja anaseama anakofia mbili.
“Moja ni mwanasheria tukasema hiyo kofia tunaiheshimu aende Kisutu kwa wanasheria wenzake, lakini akasema kofia ya pili ni mwenyekiti wa chama kwa hiyo ana uhuru na anasema CCM inaiogopa CHADEMA ndio maana inawakamata ili ishinde uchaguzi.
“Martha nataka nimuambie asikie na wanaompelekea habari kwamba nimesema hapa Tanzania kwa mwaka huu hakuna chama kinaweza kukishinda CCM, chama gani? Maana ukienda mahali ugenini ni vizuri ukajua mambo ya hapo kabla hujalalamika.
“Yeye amefika tu na ndege mara anasema CCM inaiogopa CHADEMA, chama chenyewe cha kuogopa wao wenyewe wameshagawanyika sijui kuna G55 wanatafuta chama cha kwenda anailaumu tume anasema kwa nini inawaonea Chadema.
“CHADEMA waliambiwa Aprili 12 waende wakatie saini masharti ya maadili ambayo walishapelekewa siku nyingi wao ndio walikataa kwenda lazima waanzishe zogo ili magazeti wapate cha kuandika, wakakataa kwenda sasa kama wao wana uwezo washauriane na tume sisi CCM tunawangoja.
“Tume ikikubali tuko tayari waje tumejipanga vizuri na watashindwa kama walivyoshindwa sertikali za mitaa, na safari hii anasema Martha Karua kwa nini hatiuzungumzi nao, nani anakataa kuzungumza nao? CCM hatuogopi,” alisema.
Hata hivyo alisema demokrasia ya kuchochea watu wagome uchaguzi ni kupinga haki za wengi kwa sababu wengi wanataka kupiga kura lakini CHADEMA inadai kuwa na haki ya kuzuia hivyo alihoji hiyo ni demokrasia?.