MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza na Bi Neema Simba mkazi wa Kibaigwa akiwakatika maandalizi ya Kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Kibaigwa alipotembelea Hodi ya Wazazi.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza na Neema mayai mkazi wa Mlali akiwakatika maandalizi ya Kujifungua katika hospitali ya Wilaya ya Kibaigwa alipotembelea Odi ya Wazazi.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akikagua Maendeleo ya Ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya Kongwa akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkoa wa Dodoma.
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Stephen Wasira, akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, akiwa katika ziara ya kukagua uhai wa Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi Mkoa wa Dodoma.
………………..
*Ataka itumike vizuri kujadiliana, kujenga hoja ili kuleta maelewano
*Ataka isitumika kuchochea shari kama wanavyofikiri baadhi ya wanasiasa
Na Mwandishi Wetu, Kongwa
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara Stephen Wasira, amesema maana ya demokrasia ni majadiliano, hoja na maelewano kwa lengo la kuimarisha umoja na ushirikiano katika kujenga taifa.
Amesema demokrasia sio vurugu kama ambavyo baadhi ya wanasiasa hususan wa vyama vya upinzani wanavyofikiri na kupiga kelele kutaka shari jambo ambalo CCM haikubaliani nalo.
Wasira alieleza hayo jana wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma akiwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020-2025 ikiwa sehemu ya shughuli za kuelekea maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Tanzania ambao uliingiwa Aprili 26, mwaka 1964.
“Kama una hoja za kuwashawishi wapigakura wakukubali toa, kama huna kubali….kwa sababu hawana watu, uchaguzi wa serikali za mitaa wameshindwa kwa sababu hawana wagombea, sasa wanalalamika tumeibiwa mumeibiwa wapi?
“Vijijini humo hawana watu, hata mkienda kwenye kijiji cha Kongwa mkasema niitieni hata watu 10 wa CHADEMA nitakulipa, mtu atapata tabu sana na atakosa hela maana hawapo.
Alisema kutokana na kutokuwa na wananchi wanaowaunga mkono ndiyo maana wapinzani walishindwa kufanya vizuri katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
“Sasa wewe ukose asiliamia 60 ugombee asilimia 40, uweke watu hawana sifa, ushindwe halafu uende Umoja wa Mataifa, huko utaenda lakini sisi tutakuwa tumeshamaliza hiyo kazi.
Wasira alisema CCM ina ajenda ya kudumu ya kubadili maisha ya watu, yawe mazuri kila mwaka, ya leo yawe mazuri kuliko jana na ya kesho yawe mazuri kuliko ya leo.
Kwa upande wake Spika Mstaafu wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa, Job Ndugai alisema kutokana na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan CCM katika jimbo hilo na mkoa mzima wa Dodoma haina kizingiti cha kushinda uchaguzi mkuu ujao.
Spika Mstaafu Ndugai alisema kuwa Kongwa ni kitovu cha uimara wa Chama na kwamba kutokana na kazi nzuri hata uchaguzi ukiitishwa sasa ushindi utapatikana kwa kishindo.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene alisema ziara hiyo ya Wasira katika mkoa huo ni ya kiserikali kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ilani na kukagua maendeleo yanayoletwa na serikali ya CCM.
Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule alisema katika kipindi cha miaka minne minne serikali imefanya kazi kubwa hususan kujenga miradi ya maendeleo ambayo inawagusa wananchi moja kwa moja.
Akitolea mfano wa Kongwa alisema moja ya miradi hiyo ni hospitali ya wilaya hiyo ambayo imeleta ahueni kubwa kwa wananchi.