Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Rais wa Taasisi ya Fedha ya Kimataifa ya Benki ya Dunia (IFC), Bw. John Gandolfo, katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Tanzania, jijini Washington D.C., Marekani.
Katika mazungumzo hayo, walijadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuongeza upatikanaji wa mitaji na mikopo kwa sekta binafsi, ufanisi na maendeleo ya masoko ya fedha na mitaji, pamoja na fursa za uwekezaji nchini Tanzania.
Gavana Tutuba alieleza kuwa uchumi wa Tanzania ni imara na thabiti, jambo linalodhihirishwa na viashiria mbalimbali vya kiuchumi. Alitoa wito kwa IFC pamoja na mashirika mengine ya kimataifa kuwawezesha kifedha wawekezaji wote wenye nia ya kuwekeza nchini Tanzania.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Gavana, Dkt. Yamungu Kayandabila, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi BoT, Dkt. Suleiman Missango, Meneja wa Sera ya Fedha BoT, Bi. Asimwe Bashagi, pamoja na maafisa waandamizi kutoka IFC.