Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati wa Mkutano wa Magavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika Nchi za Afrika Kundi la Kwanza (Africa Group I Constituency – IMF), ikiwa ni sehemu ya mikutano ya majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, inayoendelea jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo alizishauri nchi za Afrika kuweka mikakati ya kufanya uwekezaji na biashara ndani ya Bara la Afrika ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sera za kiuchumi zinazojitokeza hivi sasa.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb)(kulia), akizungumza wakati wa Mkutano wa Magavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) katika Nchi za Afrika Kundi la Kwanza (Africa Group I Constituency – IMF), ikiwa ni sehemu ya mikutano ya majira ya Kipupwe ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia, inayoendelea jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo alizishauri nchi za Afrika kuweka mikakati ya kufanya uwekezaji na biashara ndani ya Bara la Afrika ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sera za kiuchumi zinazojitokeza hivi sasa. Kushoto ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington D.C, Marekani)
…………………
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amezishauri nchi za Afrika kuweka mikakati ya kufanya uwekezaji na biashara ndani ya Bara la Afrika ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya sera za kiuchumi zinazojitokeza hivi sasa duniani.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa ushauri huo jijini Washangton D.C, nchini Marekani, wakati akichangia taarifa ya Mwaka ya utekelezaji ya majukumu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), wakati wa Mkutano wa Majira ya Kipupwe (Spring Meetings) wa Magavana wa Shirika hilo wa Nchi za Afrika Kundi la Kwanza (Africa Group I Constituency – IMF).
Alisema kuwa mabadiliko ya kisera yanayojitokeza hivi sasa duniani ikiwemo vikwazo vya kibiashara vinavyotolewa na mataifa makubwa kwa kuongeza ushuru na tozo mbalimbali, iwe ni chachu kwa nchi za Afrika kutafuta njia za kujiimarisha kiuchumi kwa kuweka mipango madhubuti katika bajeti za nchi na kuuziana bidhaa.
Dkt. Nchemba alisisitiza kuwa hali ilivyo sasa inaonesha nchi za Afrika zinakuwa washindani wa kibiashara badala ya kuwa washirika hali inayotishia mustakabali wa kiuchumi wa nchi hizo.
Alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuangalia maeneo ya uwekezaji katika miundombinu mbalimbali ndani ya Bara hilo ikiwemo ujenzi wa viwanda vya kutengeneza dawa muhimu za binadamu na sekta nyingine zitakazochangia kukuza ajira kwa wananchi wao pamoja na kuimarisha uchumi wa nchi hizo.
Mhe. Dkt. Nchemba alisema kuwa ufinyu wa ufadhili wa kimataifa, unaochochewa na kupanda kwa viwango vya riba katika nchi zilizoendelea kiuchumi na kuhama kutoka kutoa misaada na ukopeshaji wa masharti nafuu, kumezuia zaidi nafasi ndogo ya kifedha katika nchi hizi kujiletea maendeleo.
Aliongeza kuwa matokeo yake, kuyumba kwa uchumi mkuu kumeongezeka, uwezo wa kitaasisi umemomonyoka, na upatikanaji wa ufadhili wa masharti nafuu na wa soko umezidi kuwa na vikwazo, na kudhoofisha matarajio ya kufikia maendeleo yanayotarajiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Botswana, Bw. Cornelius Dekop, aliunga mkono ushauri wa Tanzania na kusisitiza kuwa uchakataji wa bidhaa ndani ya nchi za Afrika pamoja na ushirikiano wa kibiashara, utakuwa na tija kubwa kuliko utegemezi wa biashara nje ya mipaka ya Afrika.
Alisisitiza kuwa changamoto za kibiashara zilizopo hivi sasa katika dunia itumike kama fursa ya kuliamsha Bara la Afrika kutafuta njia za kujiimarisha kiuchumi kwa kuwa katika Bara hilo kuna soko kubwa na pia fursa za uwekezaji na biashara kwa ujumla.
