Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (kushoto), akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse, baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika ya Tanzania na Shirika hilo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (katikati), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) (kulia), na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika ya Tanzania na Shirika hilo.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (katikati), Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb) (wa tatu kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse (wa tatu kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (wa pili kulia), Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil (wa kwanza kushoto), na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Dkt. Fred Msemwa, wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukutana na kufanya mazungumzo kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano katika ya Tanzania na Shirika hilo. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Washington)




…….
Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amesema kuwa Tanzania imejipanga kukabiliana na mabadiliko ya sera za nje za Marekani kuhusu misaada kwa nchi za Afrika kwa kutumia rasilimali zake ndani kupitia Bajeti Kuu ya Serikali.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse, kando ya Mikutano ya Majira ya Kipupwe ya IMF na Benki ya Dunia, inayofanyika Jijini Washington D.C, nchini Marekani.
Dkt. Nchemba alikuwa akijibu swali la Bw. Ubisse, aliyetaka kufahamu mipango ya Serikali ya kukabiliana na uamuzi wa Marekani wa kusitisha misaada yake kwa Bara la Afrika ikiwemo sekta ya afya pamoja na kuweka ushuru wa bidhaa zinazoingizwa nchini humo kutoka mataifa hayo na mengine duniani kote.
Alisema kuwa Serikali imetenga fedha na kuongeza mafungu ya matumizi kupitia Bajeti Kuu ya Serikali ya Mwaka wa Fedha 2025/2026, kwa ajili ya kugharamia sekta mbalimbali zinazoathiriwa moja kwa moja na uamuzi huo wa Marekani, ikiwemo sekta ya afya.
Dkt. Nchemba alifafanua kuwa Serikali imejipanga kubana matumizi yake ya kawaida na kuelekeza fedha nyingi katika maeneo ya huduma za jamii na sekta za uzalishaji ili kulinda uchumi wa nchi unaokua kwa kasi lakini pia kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma muhimu za kijamii.
“Nchi zetu za Afrika, Tanzania ikiwemo, hatuwezi kuruhusu dira yetu ya maendeleo ikakwazwa na mabadiliko ya kisera ya mataifa mengine, tutachukua hatua Madhubuti za kutenga fedha kwa ajili ya huduma za jamii, kukuza uzalishaji pamoja na ujenzi wa miundombinu ambapo tutapitia upya eneo la matumizi na mapato ya serikali” alisema Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, alisema kuwa Serikali imekamilisha Dira Mpya ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, ambayo imeweka misingi ya kukuza uwezo wa nchi kujitegemea kwa kuimarisha sekta muhimu za uzalishaji, ikiwemo kilimo, matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, hatua itakayokuza kipato cha mtu mmoja mmoja na uchumi wa taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa kupitia Dira hiyo itakayoanza kutumika kuanzia mwaka wa fedha 2025/2026, ambayo hivi sasa inaandaliwa mpango wa utekelezaji wa mwaka mmoja mmoja, utaongeza uwezo wa kipato cha Mtanzania, kwa mwaka, kutoka dola za Marekani 1,250 za sasa hadi kufikia dola 4,700 ifikapo mwaka 2050.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Kwanza la Nchi za Afrika wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Bw. Adran Ubisse, aliipongeza Tanzania kwa kuchukua hatua hizo madhubuti za kusimamia uchumi na kuhakikisha kuwa sera za nje za misaada za mataifa mengine haziathiri mustakabali wa maendeleo ya nchi na huduma za kijamii kwa ujumla.
Alisema kuwa IMF inakuna kichwa namna ya kuyasaidia mataifa mbalimbali ya Afrika kuwa na sera na uwezo wa kuhimili mikikimikiki hiyo kupitia program mbalimbali zinazosimamiwa na Shirika lake ikiwemo kujiandaa na maombi mengi ya fedha yanayotarajiwa kuwasilishwa na nchi mbalimbali ili yawe na uwezo wa kujiimarisha kiuchumi.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye ni miongozi mwa Magavana wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) na Benki ya Dunia yam waka 2025,, Taasisi ambazo Tanzania inamiliki hisa, anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mikutano hiyo ya Majira ya Kipupwe (The IMF and World Bank Spring Meetings 2025).
Viongozi wengine alioambatana nao ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo (Mb), Magavana Mbadala wa IMF na Benki ya Dunia, ambao ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, Katibu wa Baraza la Mawaziri, Bw. Nsubili Joshua na Mshauri wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa masuala ya uchumi, Dkt. Blandina Kilama
Wengine ni Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango-Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Fred Msemwa na baadhi ya Wakuu wengine wa Taasisi za Serikali.