…….
Na Sixmund Begashe
Timu ya Wanawake ya mchezo wa kuvuta kamba ya MNRT Sports Club ya Wizara ya Maliasili na Utalii, imeiburuza vikali 2-1 timu ya TAMISEMI wanawake katika mchezo wa marudiano uliofanyika leo Mkoani Singida kwenye mashindano ya Maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi Duniani (MEI MOSI 2025).
Wakizungumzia michezo hiyo inayoshika kasi Mjini Singida, mashabiki mbalimbali wamesikika wakisema kuwa mashindano ya mwaka huu yamekuwa na mvuto mkubwa kutokana na timu za Wizara hiyo inayojishighulisha na Uhifadhi na Utalii nchini kuwa moto mkali kwa timu zingine pinzani.
“Hawa wachezaji wa Maliasili, sijui mwaka huu wamekula nini, wamekuwa na nguvu zaajabu mithili ya tembo wa Tarangire, hii inatupatia rahaa sana, wameleta changamoto kubwa kwa timu pinzani” alisema Bw. Ally Ramadhan, mkazi wa Gidasi Manyara.
Katika mchezo uliochezwa jana jioni timu ya Mpira wa Miguu wanaume iliwalegezea nguvu wapinzani wao timu ya Ardhi na kuwapa heshma ya sare (0-0), huku Mwenyekiti wa Club hiyo Bw. Gervas Mwashimaha, amesema bahati ya zawadi ya Sikukuu ya Pasaka waliyoipata timu ya Ardhi isitegemewe kwa timu nyingine yeyote kwenye michezo hiyo itakayofikia kilele chake siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi 2025 Mkoani Singida.