Naibu Waziri Wizara ya Sheria na Katiba Mhe. Jumanne Sagini wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa mawakili wa serikali jijini Dodoma.
Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno akiwapa ujumbe viongozi wapya wa Chama cha Mawakili wa serikali mara baada ya kuapishwa rasmi kuanza majukumu yao.
Rais mpya wa Chama cha Mwakili wa serikali Bavoo Junus akiwashukuru wajumbe wa mkutano Mkuu huo kwa kumuamini na kumchagua.
……….
Dodoma
Naibu Waziri Wizara ya Sheria na Katiba Mhe. Jumanne Sagini , amewataka mawakili wa serikali kuendelea kufanya kazi zao kwa weledi na kuhakikisha uzoefu wao unasaidia kuimarisha utawala wa sheria katika utekelezaji wa majukumu yao, ili kufanikisha malengo ya Taifa kupitia Dira ya Maendeleo 2050.
Mhe. Sagini ametoa wito huo jijini Dodoma wakati akifunga mkutano mkuu wa chama cha mawakili wa serikali.
Amesema taaluma ya sheria ni ya kipekee, si kwa sababu ya historia yake pekee bali kutokana na umuhimu wake katika kila nyanja na sekta, kwani hakuna sekta inayoweza kufanya kazi bila sheria na miongozo mahsusi.
Ameeleza kuwa mchango wa wanasheria ni muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa, na kwamba elimu yao inapaswa kuonekana katika maboresho ya sheria na mifumo ya kisheria ili kukuza uchumi, kuchochea maendeleo ya wananchi na kuimarisha huduma za kijamii zinazotegemea sheria mahsusi.
“Nategemea kuwaona mawakili wa serikali wakisaidia Serikali katika usuluhishaji wa migogoro ya kitaifa, kulinda rasilimali za Taifa letu kwa kutumia taaluma yenu ya sheria na kutekeleza haki kwa kalamu zenu,” amesema. Mhe Sagini.
Aidha, amewataka waendelee kuwa waadilifu katika kazi zao na kuzingatia weledi, ili kujenga imani kwa wananchi juu ya huduma wanazozitoa na hivyo kusaidia kuimarisha utulivu wa kijamii.
“Waendelee kujiendeleza kitaaluma, hasa katika maeneo ya sheria za ndani na za kimataifa, sambamba na kuongeza maarifa katika maeneo mapya yanayojitokeza katika dunia ya sasa,” alisisitiza.
Naibu Waziri Sagini amepongeza pia kuwepo kwa kitengo cha utafiti na mafunzo katika muundo mpya wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambacho kitasaidia kuongeza tija katika kujiongezea maarifa kwa wanachama wa chama hicho.
“Viongozi mliochaguliwa, hakikisheni mnarudisha imani ya wanachama kwa kufanya kazi kwa weledi, maarifa na ubunifu, na kuendeleza mazuri yote yaliyofanywa na uongozi uliopita,” ameongeza.
Pia, amewataka mawakili wa serikali kushiriki kikamilifu katika kampeni ya Mama Samia Legal Aid, ambayo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi, pamoja na kliniki za kisheria zinazoratibiwa na ofisi yake, ambazo zimekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi.
“Kila wakili wa serikali anapaswa kufanya kazi kwa weledi na uadilifu kwa mujibu wa sheria na misingi ya taaluma yao, kwa maslahi ya Taifa na haki za wananchi,” amefafanua.
Amesisitiza pia umuhimu wa wakili wa serikali kushiriki kikamilifu katika kuzuia mashauri dhidi ya serikali kwa kutoa ushauri stahiki mapema, badala ya kusubiri kuitetea serikali mahakamani.
Kwa upande wake, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Samweli Maneno, amesema viongozi wapya waliochaguliwa watawajibika kwa viapo vyao na kuhojiwa kuhusu ahadi walizotoa wakati wa kampeni.
Ameongeza kuwa viongozi hao wataongoza kwa mwaka mmoja na watapimwa kwa utekelezaji wa mipango iliyopo katika mpango mkakati wa chama kwa mwaka wa kwanza.
Naye Rais mpya wa chama hicho, Bavoo Junus, amesema wana jukumu la kujenga na kuimarisha chama chao ili kifikie malengo na matarajio ya kila mwanachama.