Na
Neema Mtuka Sumbawanga,
Rukwa. MKUU wa wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa ameitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilaya ya Sumbawanga kuchunguza tuhuma zinazomkabili mganga mfawidhi wa kituo cha afya Milepa John Minde akituhumiwa na wananchi kwa kuwatoza fedha za matibabu zaidi ya kiwango kilichowekwa na serikali na kutowapa stakabadhi ya malipo.
Hayo yamesemwa leo April 17,2025 na mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan.
Akitoa maelekezo kwa TAKUKURU mara baada ya wananchi kutoa kero zao katika mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika kijiji cha Kinambo kata ya Milepa Nyakia amesema hakuna kiongozi anayetakiwa kuwanyanyasa wananchi kila kiongozi yupo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
“Wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi hivyo hawana sababu ya kutoa huduma wanavyojisikia wao wanapaswa kutoa huduma kwa upendo na sio kuwaumiza wagonjwa.Nyakia amefafanua
Nyakia amewataka watumishi wa serikali kufanya kazi kwa weredi na kufuata sheria kanuni taratibu na miongozo ya kiutumishi bila kubagua wala kumwangalia mtu wa kumuhudumia usoni ni wajibu wao.
Aidha amesema serikali inapambana kuhakikisha huduma za kijamii zinapatika karibu na maeneo ya wananchi na kuwataka wananchi kuendelea kufichua mambo yanayofanywa na wahudumu mbalimbali wa afya.
“TAKUKURU mchunguzeni huyu daktari haiwezekani wananchi wote wanamsema yeye tu haiwezekani hakikisheni mnamchunguza na mkurugenzi amuondoe na kumletea daktari mwingine hapa TAKUKURU wanapofanya kazi yao.” Amesema
Amesema lengo la Serikali ni kuona wananchi wanapata huduma wanayostahili kwa kuwa vituo vya afya vinajengwa kwa kodi zao.
“Watumishi acheni kuwanyanyasa wananchi mishahara yenu mnalipwa kwa kodi za hawa wananchi “amesisitiza Nyakia.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Milepa Apolinari Macheta amekili kuwa tuhuma hizo ni za kweli ambapo baraza la kijiji walikaa na kujadili pamoja na kupata vithibitisho kwa baadhi ya wananchi waliochukuliwa fedha zao na hawakupewa risiti ya malipo baada ya kulipia huduma za matibabu katika kituo cha afya Milepa.
” Tumepata uthibitisho kwa wananchi walioombwa fedha zaidi ya gharama iliyopo watu watatu mmoja anaitwa tumaini ni mlemavu wa ngozi (albino)aliombwa kiasi cha sh.200,000 alipojaribu kuomba kupunguziwa aliambiwa atoe sh.80,000 ambapo alitoa sh.50,000 na hakupewa lisiti,mwingine aliombwa sh.25,000 na mwingine sh.15,000 akidai ni fedha za awali kabla hujaanza matibabu na wote hawa hakuna aliyempa risiti inayoonyesha amelipia matibabu” amesema Macheta.
Nao baadhi ya wananchi akiwemo Moreen Kipeta ameipongeza serikali ya awamu ya sita kwa kazi nzuri ambayo wameendelea kuifanya katika maeneo mbalimbali katika kata yao ya milepa hususani katika bonde la ziwa Rukwa kwa kujenga madaraja ambayo yamekuwa yakisombwa na mvua mara kwa mara.
Amesema kumekuwa na huduma nzuri za kijamii zinazotolewa ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wakitembea umbali mrefu kufuata matibabu.
“Ninaiomba serikali kutuletea umeme katika kitongoji cha Unyele ambapo kitongoji hicho ndicho kitongoji pekee ambacho bado hakijafikiwa na umeme katika kata ya Milepa.”amesema kipeta