Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Same Mhe. Kasilda Mgeni amewasisitiza vijana waliojitokeza kwa ajili ya kuanza mafunzo ya Awali ya Jeshi la Akiba (Mgambo) kutanguliza Uzalendo, kuzingatia matumizi sahihi ya silaha, Uadilifu na kutumia vyema mafunzo watakayoyapata katika kupambana na uhalifu kwenye maeneo yao ikiwemo kupambana na Rushwa.
Mhe. Kasilda amesema hayo Aprili 16, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awali ya jeshi la Akiba (Mgambo) kundi la 29/2025 kata ya Mwembe Wilayani Same, ambapo amewasisitiza kuyatendea haki mafunzo hayo.
“Mafunzo haya ni muhimu sana hakikisheni mnayatendea haki na mnayatumia vizuri kwa kutanguliza Uzalendo, Uadilifu, zingatieni matumizi sahihi ya silaha hakikisheni hazitumiki kinyume, pia mafunzo mtakayoyapata msiende kutatumia kwenye uhalifu ninyi muwe sehemu ya kupambana na uhalifu kwenye maeneo yenu” amesema Mhe. Kasilda.
Sambamba na hayo Mhe. Kasilda amesema kuwa vijana wa Jeshi la Akiba (Mgambo) ni muhimu sana katika kulinda usalama wa maeneo mbalimbali hususani maeneo ya Viijijini huku akiwaonya wale watakaotumia vibaya mafunzo hayo kwa kufanya uhalifu kuwa watachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kuwafutia sifa za kuwa Askari wa Jeshi la Akiba (Mgambo).
Kwa upande wake Mshauri wa Jeshi la Akiba Wilaya ya Same Afisa Mteule daraja la pili Emmanuel Shija amesema kuwa masomo yatakayotolewa katika mafunzo hayo ni pamoja na Uraia, utimamu wa Mwili, kuzuia rushwa, mbinu za kivita, huduma ya kwanza, Usomaji ramani, Uhandisi pamoja na mambo mengine yanayolihusu Jeshi la Akiba.
Pia mafunzo hayo kwa vijana yatawasaidia katika kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, majanga mbalimbali ikiwemo moto, mabadiliko ya Tabianchi, uhalifu pamoja na kuwasaidia katika kujipatia kipato na ajira.
Katika mafunzo hayo ya Awali ya Jeshi la Akiba (Mgambo) kundi la 29/2025 katika wilaya ya Same hadi sasa idadi ya washiriki imefikia 87 wakiwemo wanaume 72 na wanawake 13, Aidha mafunzo hayo yanatarajia kumalizika mwezi Agosti mwaka huu.