

Na BALTAZAR MASHAKA, MOROGORO
KAIMU Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga, amewataka watumishi wa bodi hiyo kuwa wazalendo, wawajibikaji na waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku, ili kuchochea maendeleo na kuleta mabadiliko chanya ndani ya taasisi hiyo.
Mhandisi Kalimbaga aliyasema hayo leo, katika kikao kazi cha siku tatu kinachoendelea mkoani Morogoro, kikilenga kuboresha utendaji kazi wa taasisi hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya watumishi na idara mbalimbali ili kufanikisha malengo ya Mfuko wa Barabara.
“Ni wajibu wa kila mtumishi kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya taasisi yetu. Tukiwa na mshikamano, uwajibikaji na uadilifu, tunaweza kufanikisha malengo tuliyojiwekea kwa ustawi wa taasisi na taifa kwa ujumla,” alisema Mhandisi Kalimbaga.
Katika kikao hicho, mada mbalimbali zitawasilishwa zikiwemo elimu ya utunzaji wa siri za serikali, afya ya akili, pamoja na masuala yahusuyo utumishi wa umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Rasilimali Watu na Utawala wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Aureus Mapunda, alisema kikao hicho ni fursa kwa watumishi kujikumbusha majukumu yao, pamoja na kupata maarifa mapya yatakayosaidia kuboresha utendaji kazi.
“Kikao hiki siyo tu kinatupatia mwanga juu ya majukumu yetu, bali pia kinatufanya kutathmini utendaji wetu na kuona maeneo yanayohitaji kuboreshwa,” alisema Mapunda.
Naye Hindu Mussa, mmoja wa watumishi wa Mfuko wa Barabara, ameishukuru bodi hiyo kwa kuandaa kikao hicho, akisema kimetoa nafasi kwa watumishi kuimarisha uelewa wao kuhusu wajibu wao kwa umma na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zikiwemo za afya ya akili.