Msemaji wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi kuwa lengo la klabu hiyo si kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, bali kutwaa ubingwa wa bara hilo. Akiwa visiwani Zanzibar, Ahmed amesema mashabiki wa Simba hawapaswi kuridhika na nafasi ya nne au hatua ya nusu fainali kwani malengo ya Simba ni makubwa zaidi.
“Nafasi ya nne Afrika bado sio malengo ya Simba, nusu fainali bado sio malengo, ni sehemu ya mapito. Tunaitaka nafasi ya kwanza Afrika,” alisema.
Ahmed Ally pia amewahakikishia mashabiki kuwa mabadiliko ya uwanja wa mchezo dhidi ya Stellenbosch FC kutoka Benjamin Mkapa hadi Amaan, Zanzibar hayana athari kwa morali ya timu.
“Kanzu ndio imebadilika lakini sheikh ni yule yule. Mnyama ni yule yule na malengo yetu ni yale yale — kumfanya vibaya Stellenbosch FC,” alisema huku akiwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi na kuja “kupiga kelele”.
Ahmed amesema siku ya mchezo, ambayo itaangukia Pasaka, milango ya uwanja itakuwa wazi kuanzia saa 5 asubuhi, na kutakuwa na burudani maalum kwa mashabiki.
“Moja ya silaha ya kuwachanganya Stellenbosch ni kelele. Uwanjani tunataka sauti na nguvu, kila anayekuja ajiandae kupiga kelele.”