FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Wakazi zaidi ya 12,000 wa vijiji vya Alabama na Mizani, Wilaya ya Malinyi, wameondokana na adha ya upatikanaji wa maji safi na salama kufuatia kukamilika kwa Mradi wa Maji wa Mizani-Itete, unaotekelezwa na Serikali kupitia Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Mradi huo ni miongoni mwa miradi iliyozinduliwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025 na umegharimu zaidi ya shilingi milioni 321, fedha zilizotolewa kupitia mpango wa “Lipa kwa Matokeo (PForR).”
Kwa mujibu wa Meneja wa RUWASA Wilaya ya Malinyi, Marco Chogelo, utekelezaji wa mradi wa Maji Mizani-Itete ulianza mwezi Februari 2024 na kukamilika mwezi Novemba mwaka huo huo.
Mradi huo umehusisha uchimbaji wa mitaro, ulazaji wa mabomba yenye urefu wa kilomita 8.2, ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji, ujenzi wa nyumba ya mitambo (power house), pamoja na ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lenye uwezo wa lita 200,000.
Wakazi wa Kijiji cha Mizani, Kata ya Itete, wamesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kumeimarisha shughuli zao za kiuchumi kwani awali walilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji safi na salama kwa matumizi ya kila siku.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2025, Ismail Ali, aliipongeza RUWASA kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha huduma ya maji safi na salama inawafikia wananchi wa vijijini.
“Niipongeze sana RUWASA kwa kazi kubwa mnayoifanya. Mmekuwa wakombozi wa wananchi katika suala zima la upatikanaji wa maji safi na salama vijijini,” alisema Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025.