Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab akizungumza na Madereva wa Wizara hiyo kuhusiana na nidhamu huko Ofisini kwake Migombani, Wilaya ya Mjini.
Dereva kutoka Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamuduni Mussa Abdalla Mussa (Mussa Fujo) akitoa neno la shukrani mara baada ya kumaliza mafunzo ya nidhamu kwa madereva wa Wizara hiyo huko Migombani Wilaya ya Mjini.
Dereva Hilali Talib Aboud wa Baraza la Kiswahili Zanzibar, akiiomba Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutengewa fungu maalum kwa ajili dharura wakati inapojitokeza huko Migombani Wilaya ya Mjini.
Dereva Mohamed Omar kutoka Tume ya Utangazaji Zanzibar, akitoa maelezo mbele ya Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab huko Ofisini kwake Migombani Mjini Zanzibar.
Baadhi ya Madereva wa Wizara ya Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo wakimsikiliza kwa makini Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara hiyo Migombani Wilaya ya Mjini.
Picha ya pamoja ya Madereva wa Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo mara baada ya kumaliza kikao na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Hamad Rajab huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini.
………
Madereva wa Wizara ya Hbari, Vijana, Utamaduni na Michezo wametakiwa kufuata taratibu, Kanuni na Sheria za Utumishi ili kuondosha malalamiko kwa baadhi ya Viongozi.
Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Fatma Hamad Rajab ameyasema hayo huko Ofisini kwake Migombani Wilaya ya Mjini wakati alipokuwa akizungumza na Madereva wa Wizara hiyo.
Amesema baadhi ya Madereva wanakiuka mipaka ya kazi zao kwa kutoa siri na kutumia lugha chafu kwa Viongozi jambo ambalo ni kinyume na madili ya kazi.
Aidha amewataka Madereva hao, kudumisha nidhamu, Upendo na Mshikamano ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Amefahamisha kuwa, hali hiyo itawajengea sifa nzuri ya uwajibikaji na utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Aidha amesema baadhi ya Madereva wanakwenda katika vituo vya kutia mafuta (Sheli) wakiwa na Viongozi jambo ambalo linaharisha usalama wa maisha yao.
‘’Kwa wenzetu Tanzania bara huoni Dereva kutia mafuta wakati akiwa na bosi wake lakini hapa petu, Madereva wanatia mafuta, wanachati na kuongea na Simu bila wasiwasi wowote’’alisema Katibu Fatma.
Hata hivyo amewataka Madereva hao, kuwa makini na kufuata Sheria wakati wanapokuwa Barabarani ili kujikinga na matatizo yanayoweza kujitokeza ikiwemo kupata ajali.
‘’Ukikamata Sukani ujuwe, umebeba roho ya mtu lazima akili yako iwe imetulia vizuri barabarani ili usije kusababisha majanga ‘’ alibainisha Katibu huyo.
Mbali na hayo amewataka, kuzifanyia matengenezo gari za Serikali kwa wakati ili ziweze kufanya kazi kwa ufanisi na kudumu kwa muda mrefu.
‘’Gari za Serikali muzionee huruma, muzithamini na muzijali ili zibaki katika hadhi nzuri na pia muzifanyie matengenezo kwa muda unaotakiwa’’ alilisitiza Kiongozi huyo.
Pamoja na hayo amewaahidi Madereva wa Wizara hiyo, kuwasimamia ili kuhakikisha wanapata haki zao na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo Mafunzo.
Nao Madereva wa Wizara hiyo akiwemo Mussa Abdalla Mussa (Mussa fujo) kutoka Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamuduni Zanzibar, Mohamed Omar wa Tume ya Utangazaji Zanzibar na Hilali Talib Aboud kutoka Baraza la Kiswahili Zanzibar wameiomba Wizara hiyo kuwatengea fungu la dharura ili liweze kuwasaidia wanapopata matatizo.
Aidha wamesema wamefarajika sana kutokana na mafunzo hayo na kuahidi kuyafanyia kazi maagizo waliopewa sambamba na kuomba kuendelea kupatiwa fursa mbalimbali zilizopo ili kuongeza motisha katika sehemu ya kazi.