Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja akizungumza wakati wa Kikao cha Uwasilishaji wa Taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mazingira katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025.
Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Kemilembe Mutasa akito neno la utangulizi wakati wa Kikao cha Uwasilishaji wa Taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mazingira katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja (katikati waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi pamoja na washirki wa Kikao cha Uwasilishaji wa Taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mazingira katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025.
Washiriki wakiwa katika Kikao cha Uwasilishaji wa Taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mazingira katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025.
…………..
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja amewataka Maafisa Mazingira wa mikoa kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha wananchi kutunza mazingira.
Amesema hayo wakati wa Kikao cha Wataalamu wa Mazingira Uwasilishaji wa Taarifa ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Mazingira katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kilichofanyika jijini Dodoma leo tarehe 11 Aprili, 2025.
Kikao kimewakutanisha maafisa mazingira wa mikoa yote 26 ya Tanzania Bara pamoja, maafisa viungo na Menejimenti ya Ofisi ya Makamu wa Rais wanaosimamia mikoa hiyo.
Aidha, Mhandisi Luhemeja amesema kupitia Maafisa Viungo kwa kushirikiana na Wataalam wa Mikoa husika, wana jukumu la kuibua changamoto mbalimbali za mazingira na kuainisha fursa na mikakati ya kukabiliana nazo.
Amesema katika kutekeleza jukumu hilo, Maafisa viungo husika wameweza kufanya ufuatiliaji na tathmini ya hifadhi na usimamizi wa mazingira kwa awamu tatu, ili kubaini mwenendo wa hali ya mazingira katika Wizara za Kisekta, Taasisi na Mashirika ya Umma, Sekretariati za Mikoa na Mamlaka ya Serikali za Mitaa, na kupendekeza hatua mahsusi zitakazochukuliwa kuimarisha hali ya mazingira.
Hata hivyo, Mhandisi Luhemeja amesema ukataji wa miti hovyo na uharibifu wa misitu ni mkubwa kwani takwimu zinaonesha ongezeko kubwa la uharibifu wa misitu kutoka hekta 372,816 mwaka 2019 hadi hekta 469,420 mwaka 2023 ambao ni sawa na kupoteza wastani wa hekta 24,151 kila mwaka.
“Uharibifu huu umechangiwa kwa sehemu kubwa na shughuli za binadamu zisizo endelevu ikiwemo utegemezi mkubwa wa nishati ya kuni na mkaa; uvunaji wa rasilimali misitu usioendelevu; kilimo kisicho endelevu na ufugaji holela usiozingatia uwiano wa idadi ya mifugo na maeneo ya malisho,” amesema.
Ameongeza kuwa uchafuzi wa mazingira, hususan kutokana na utupaji taka hovyo (taka ngumu, majitaka, plastiki na sumu) katika maeneo ya mijini ni takriban kiasi cha tani milioni 7 za taka ngumu huzalishwa hapa nchini kwa mwaka, ambapo wastani wa asilimia 50.
Mhandisi Luhemeja amesema maafisa mazingira wa mikoa wana jukumu la kuhakikisha wanahamasisha wananchi katika kutumia fursa za mazingira ikiwemo biashara ya kaboni kwa kupanda miti hivyo kuhifadhi mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Kemilembe Mutasa amesema hatua ya uteuzi wa maafisa viungo wa mikoa inasaidia kuimarisha masuala ya hifadhi na usimamizi wa mazingira.
Nao Maafisa mazingira wakiwemo kutoka TAMISEMI Theodory Mulokozi na Mangabe Mnilango kutoka Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti wa maafisa mazingira wa mikoa wamepongeza kuishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuandaa kikao hicho.
Wamesema kikao hicho kitasaidia kuwaleta pamoja wataalamu wa mazingira na kujadili mustakabali mzima wa mazingira kwa kizazi cha sasa na kijacho.