Katikati ya ratiba yake iliyoshehehi vikao vingi jijini Dar es Salaam leo, akitoka airport, kwenda Ikulu, vikao na jioni hii kuondoka nchini, mmoja wa wamiliki ambaye kwa sasa ndiye anasimamia uendeshaji wa klabu ya Manchester United ya Uingereza, Sir. Jim Ratcliffe, kwa mapenzi makubwa, na labda akitaka kutuma ujumbe kwa mashabiki wa timu hiyo kote duniani, alitoa heshima ya kukutana na baadhi ya mashabiki na kueleza hadithi ya mageuzi yajayo klabuni humo.
Akieleza kuanzia changamoto ya mifumo ya uendeshaji wa klabu hiyo, aina ya watendaji iliyokuwa nayo, aina ya usajili iliyokuwa ikifanya, ni kama vile Sir Ratcliffe ametoa “Tamko la Dar es Salaam” alipokuwa akijibu hoja za mashabiki hao aliposema: “ Mwezi Machi mwaka huu tumekamilisha mageuzi ya mifumo ya kiutawala na uendeshaji ndani ya klabu. Mwelekeo sasa ni mageuzi ya timu. Tusubiri kusikia usajili dirisha kubwa lijalo.”