Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa ZURA, Mbarak Hassan Haji Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kupanda kwa bei za mafuta huko ofisini kwao zura Maisara wilaya ya mjini.
……………
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) imetangaza rasmi kupanda kwa bei za mafuta, ambapo bei mpya zinatarajiwa kuanza kutumika kuanzia kesho, tarehe 9 Aprili 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja wa Kitengo cha Uhusiano wa ZURA, Mbarak Hassan Haji huko ofisini kwao zura Maisara wilaya ya mjini, amesema kuwa mabadiliko ya bei hizo yamechangiwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia pamoja na gharama za usafirishaji.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bei mpya kwa bidhaa za mafuta zitakuwa kama ifuatavyo:
Petroli, TZS 2,949 kwa lita kutoka TZS 2,939, Dizeli, TZS 3,194 kwa lita kutoka TZS 3,135, Mafuta ya Ndege TZS 2,537 kwa lita kutoka TZS 2,500 na Mafuta ya taa yatabaki kwa bei ileile ya TZS 3,200 kwa lita kwa mwezi huu wa Aprili.
Hata hivyo amesema ZURA inapanga bei kwa kuzingatia mambo mbalimbali ikiwemo Wastani wa mwenendo wa Mabadiliko ya bei za mafuta Duniani, Gharama za uingizaji wa Mafuta katika Bandari ya Tanga, gharama za mabadiliko ya fedha za kigeni zinazotumika kununulia mafuta, Gharama za Usafiri, Bima na ‘Preminium’ hadi Zanzibar, Kodi za Tozo za Serikali na Kiwango cha faida kwa Wauzaji wa Jumla na Reja Reja.
Aidha amesema Bei za Mafuta kwa Mwezi Aprili, 2025 zimeongezeka kutokana na mabadiliko ya Fedha za kigeni kwa Shilingi ya Tanzania.
Mamlaka inawahimiza Wananchi kununua Mafuta katika Vituo halali vya kuuzia Mafuta na kudai Risiti za Kielectroniki kila wanaponunua mafuta hayo ili zinapotokezea changamoto zozote wapate kusaidiwa.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (ZURA) hutangaza bei hizo za Mafuta kila ifikapo tarehe 8 ya kila mwezi.