Na Mwandishi wetu, Mirerani
SERIKALI itatoa Sh1.5 bilioni za kukamilisha jengo la sakafu tano za soko la madini ya vito lililopo eneo la Tanzanite city mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ambalo limefikia asilimia 95 kabla ya kukamilika.
Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameeleza hayo baada ya kutembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo litakaloongeza thamani ya madini ya vito pindi likikamilika.
Sendiga amesema serikali itatoa fedha hizo Sh1.5 bilioni wakati wowote ili kukamilisha soko hilo la madini ya vito lililopo eneo la Tanzanite city.
Amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza tija ya madini ya vito ikiwemo Tanzanite hivyo wadau wajipange vyema kwani jenga litakamilika hivi karibuni.
“Paliposalia ni padogo kabla ya kumalizika, wakati mkandarasi akifanya kazi kabla ya kukabidhi jengo hili ambalo litaongeza thamani ya madini kwani yatauzwa kimataifa,” amesema Sendiga.
Ametoa agizo kwa halmashauri ya wilaya hiyo kujipanga kwa kuandaa mazingira ikiwemo kupanda miti kipindi hiki ambacho mvua zinaendelea kunyesha.
Msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo Anna Akyoo amesema soko hilo limefikia asilimia 95 ya ujenzi kabla ya kukamilika kwani bado asilimia tano pekee.
Akyoo amesema thamani ya jengo hilo ni Sh5.4 bilioni na wanatarajia litakamilika mwezi huu wa Aprili mwaka 2025 na kuanza kutumika kwake.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota ameeleza kuwa watatekeleza maagizo hayo yaliyotolewa na mkuu huyo wa mkoa.
“Tumeshawaeleza wadau wa madini waanze kuchangamkia fursa ya kuwepo kwa soko hili la madini ya vito ili likikamilika washiriki,” amesema Makota.
Mdau wa madini ya Tanzanite, Rachel Njau amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaongeza thamani ya madini ya vito pindi likianza kazi na bei itakuwa juu kwani wanunuzi hadi wa kimataifa watafika.
“Tunaishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha za kujenga soko hili la madini ya vito hapa Mirerani,” amesema Njau.