Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akishuhudia utiaji saini wa Mikataba ya ushirikiano katika masuala ya ulinzi pamoja na Hati ya makubaliano kuhusu kukuza Uwekezaji pamoja na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço katika Ikulu ya Luanda nchini Angola tarehe 08 Aprili, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Angola Mhe. Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço wakizungumza katika mkutano wa Waandishi wa Habari uliofanyika katika Ikulu ya Luanda nchini Angola tarehe 08 Aprili, 2025.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akilihutubia Bunge la Jamhuri ya Angola Jijini Luanda katika muendelezo wa Ziara yake ya Kiserikali nchini humo tarehe 08 Aprili, 2025
Angola– Tanzania na Angola zimeendelea kuimarisha ushirikiano wao wa kidiplomasia na kiuchumi kupitia utiaji saini wa mikataba na hati mbili muhimu za makubaliano mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan aliye katika ziara rasmi nchini humo na Rais wa Jamhuri ya Angola, Mheshimiwa João Lourenço.
Miongoni mwa makubaliano hayo ni Rasimu ya Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Ulinzi, unaolenga kuimarisha usalama na ulinzi kwa maslahi ya pande zote mbili. Mkataba huu pia unahusisha maeneo mengine muhimu ya ushirikiano yakiwemo, Sekta ya afya, Michezo, utamaduni na jamii, Na maeneo mengine yenye maslahi ya pamoja.
Mkataba huo umewekwa kwa kipindi cha miaka mitano (5), na baada ya muda huo kuisha, pande zote zitafanya mazungumzo kwa ajili ya kuhuisha masharti ya mkataba pamoja na kuongeza maeneo mapya ya ushirikiano endapo yatajitokeza.
Mkataba huu ulisainiwa na Mheshimiwa Stergomena Lawrence Tax (Mb), Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Tamzania na Luteni General Joao Ernesto Dos Santos “Liberdade” Waziri wa Ulinzi wa Taifa na Wapiganaji wa Zamani wa Jamhuri ya Angola
Aidha, viongozi hao pia walishuhudia utiaji saini wa Rasimu ya Hati ya Makubaliano (MOU) kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Wakala wa Uwekezaji Binafsi Ukuzaji na Uwezesha Usafirisha Nje wa Angola (APEX).
Hati hii inalenga kukuza uwekezaji wa ndani na wa kigeni katika nchi hizi mbili, kwa misingi ya usawa, uaminifu, ushiriki wa hiari, na manufaa ya pamoja.
Makubaliano hayo yanalenga Kuanzisha ushirikiano wa pamoja na kwa faida kati ya taasisi hizo mbili, Kukuza ushirikiano wa kidiplomasia ili kuvutia wawekezaji, Kukuza biashara ya mauzo ya nje, Na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia.
Makubaliano haya ni ya kipindi cha miaka mitano, ambapo baada ya muda huo, tathmini na mazungumzo ya kuendeleza ushirikiano yatafanyika.
MOU hiyo imesainiwa na Bw. Gilead J. Teri, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Bw. Arlindo das Chagas Rangel Rais wa Wakala wa Uwekezaji Binafsi Ukuzaji na Uwezesha Usafirisha Nje wa Angola (APEX).
Hafla hii muhimu imeonesha dhamira ya dhati ya Tanzania na Angola katika kujenga na kuendeleza mahusiano ya karibu yenye manufaa ya pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pia amelihutubia Bunge la Jamhuri ya Angola Jijini Luanda katika muendelezo wa Ziara yake ya Kiserikali nchini humo tarehe 08 leo Aprili, 2025.