***********
Na Mwandishi wetu – Singida
Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuimarisha Sekta ya Utalii, kwa kuweka mikakati mbalimbali ya kuchechemua ongezeko la watalii na kukuza pato la Taifa kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Utalii (TDL).
Akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao kazi cha viongozi wa Taasisi za Wizara hiyo zinazotekeleza miradi kupitia mfuko huo, Mkoani Singida, Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. Abdullah Mvungi amesema kikao hicho kimelenga kupata uelewa wa pamoja wa uboreshaji wa mipango na mikakati ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati inayolenga kutoa matokeo chanya kwa jamii.
Bw. Mvungi amesema kuwa Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa vitendo kukuza utalii kupitia Mfuko huo hivyo ni vyema kwa Viongozi wa Taasisi zinazotekeleza miradi kupitia Mfuko huo kuhakikisha wanasimamia kikamilifu miradi itakayotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Aidha, Bw. Mvungi ameongeza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo umelenga kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wale wa nje, kuongeza mapato ya fedha za ndani na za kigeni, kuongeza ajira pamoja na kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia Sekta ya Utalii.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. John Mapepele ameeleza kuwa Wizara itaendelea kutoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya mafanikio yanayopatikana katika miradi.