Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile wakati akizungumza na mkandarasi
Picha na Neema Mtuka
……,…………..
Na Neema Mtuka sumbawanga
Rukwa:Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Nyakia Ally Chirukile, amewataka wakandarasi kufanya kazi kwa weredi na kuacha tabia ya kwenda kinyume na taratibu zulizopo.
DC Nyakia ameyasema hayo akiwa katika ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya Programu ya TACTIC inayotekelezwa ndani ya Manispaa ya Sumbawanga.
Akizungumza leo April 8,2025 Nyakia amesema kumekuwa na kusuasua kwa miradi jambo linalokwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo mbalimbali
Katika ziara hiyo, Nyakia amebaini uwepo wa wizi wa vifaa vya ujenzi ambapo amekemea vikali tabia hiyo kuwa inarudisha nyuma maendeleo.
“Fanyeni kazi kwa uaminifu ukiiba vifaa vya ujenzi unamkomoa nani ili hali maendeleo ni ya kwetu wote.”amesema Nyakia.
Katika ziara hiyo Dc Nyakia ameambatana na Mkurugenzi wa Manispaa Pendo Mangali pamoja na baadhi ya wataalamu, ambapo ametembelea na kukagua hatua ya umaliziaji wa jengo la mhandisi mshauri, ujenzi wa barabara za kiwango cha lami zenye urefu wa kilomita 13.03, pamoja na ujenzi wa soko la kimataifa la mazao Kanondo.
Ambapo amewasisitiza wakandarasi kuhakikisha wanatekeleza kazi kwa kasi inayotakiwa huku wakizingatia ubora, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwahudumia wananchi kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.
Aidha, amewataka wananchi kutunza miundombinu inayojengwa kwa kuhakikisha usafi wa mazingira hususani mitaro na barabara, na kuepuka uharibifu wa aina yoyote.
Nyakia amesisitiza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara za mjini ni hatua muhimu ya maendeleo, kwani Serikali inaendelea kupanga mikakati madhubuti ya kuwawezesha wananchi kunufaika kiuchumi kupitia biashara salama na endelevu katika maeneo mbalimbali ya mji wa Sumbawanga.
Naye diwani wa kata ya Mazwi Daudi Masoud amesema wananchi wanahitaji kuona maendeleo kwa vitendo na ndio maana Rais wa jamhuri ya muungano wa tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa pesa kwa lengo la kuhakikisha miradi ya maendeleo inakamilika kwa wakati.
Baadhi ya wananchi wa kata ya Mazwi akiwemo Sostenes Rupia amempongeza Mbunge wa Jimbo la Sumbawanga Mjini kwa jitihada zake za kuwatetea na kuwawakilisha vyema bungeni.
“Juhudi za mhe mbunge akiwa bungeni ambapo alikuwa akiongelea kero mbalimbali za wakazi wa Sumbawanga ndio zimezaa matunda haya tunayoyaona ya viwango vya lami za mjini soko la kimataifa na uwanja wa ndege unaoendelea kujengwa” amesema.