Marehemu Bi. Khadija Abbas Rashid alizaliwa tarehe 23 Oktoba, 1949 na kupata elimu ya msingi katika Shule ya Wasichana ya Forodhani iliyopo Unguja, Zanzibar.
Alipita katika mchujo wa vijana 100 kutoka Zanzibar ambao waliungana na wenzao kutoka iliyokuwa Tanganyika ambapo waliteuliwa kushiriki la kuchanganya udongo kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar tarehe 26 Aprili, 1965 mwaka mmoja baada ya kuasisiwa kwa Muungano.
Bi. Khadija ambaye alikuwa na umri wa miaka 16, alikuwa miongoni mwa vijana wa kitanzania wanne walioshiriki zoezi hilo ambapo alikabidhi kibuyu chneye udongo kwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mwalimu Nyerere alipokea kibuyu hicho na chenye udongo wa Zanzibar na kuchanganya na udongo mwingine kutoka iliyokuwa Tanganyika ambao pia uliwekwa kwenye kibuyu.
Tukio hilo lililofanyika katika Uwanja wa Taifa (sasa Uwanja wa Uhuru), pia lilishuhudiwa na Sheikh Abeid Aman Karume, Rashid Mfaume Kawawa na wengine.
Marehemu Bi. Khadija alifariki nyumbani kwake Raha Leo Mkoa wa Mjini Zanzibar tarehe 22 Agosti, 2023 na kuzikwa tarehe 23 Agosti, 2023 Bumbwini Makoba Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis ndiye aliyewaongoza viongozi na wananchi mbalimbali katika mazishi ya Bi. Khadija.
MZEE HASSAN
Mzee Hassan Omar alizaliwa Unguja na kupata elimu katika Chuo cha Ufundi Zanzibar. Akiwa chuoni aliteuliwa kuwa mmoja wa vijana wanne walioshiriki tukio la kuchanganya udongo akiwa na Khadija Abbas Rashid wote wakiwa wakiwa na umri wa miaka 16.
Mzee Omar alishirikiana na Hassaniel Mrema (kutoka Tanganyika) kushikilia chungu ambacho kilitumika katika kuchanganyia mchanga uliochukuliwa kutoka Kizimbani (Zanzibar) na mwingine Dar es Salaam (Tanganyika).
Pia, katika tukio la kupanda mti aina ya mwembe Hassan Mzee alimkabidhi Mwalimu Nyerere dumu la maji kwa ajili ya kumwagilia mti aina ya mwembe huku mwenzake Hassaniel akimkabidhi Sheikh Karume dumu la maji kwa ajili ya kumwagilia mwembe huo, tukio lililofanyika Ikulu Dar es Saalm. Mwembe huo upo hadi sasa.
Hassan Mzee alifariki usiku wa wa kuamkia tarehe 28 Agosti, 2024 na kuzikwa Kibweni Wilaya ya Magharibi “A” Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja tarehe hiyo hiyo mchana.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi aliongoza viongozi akiwemo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla na wananchi katika maziko ya Mzee Hassan Omar.