


…………
NA DENIS MLOWE IRINGA
MASHINDANO ya kugombea kombe la Vunja bei yameendelea kurindima katika viwanja mbalimbali mwishoni mwa wiki katika michezo miwili iliyopigwa katika viwanja viwili tofauti.
Mashindano hayo yenye zawadi nono ya milioni 10 kwa mshindi wa kwanza ikiwa ni zawadi kubwa katika mashindano ya ndondo kwa ukanda wa Nyanda za Juu na kufadhiliwa na kampuni ya Vunja Bei chini ya Fred Ngajilo.
Katika mchezo wa kwanza kati ya timu ya Walimu Fc dhidi ya Dream Boys Fc mchezo ulimalizika kwa kutoka sare ya mabao 2- 2.
Katika mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa shule ya msingi Mlandege timu ya Walimu Fc ilikuwa ya kwanza kupata goli lilofungwa na Almas Mlelwa katika dk 13 na Shodan Vaginga aliwapatia goli la pili Walimu fc katika dk 24.
Katika dk ya 36 Antony Mtelewe aliwapatia goli la kwanza Dream fc na kufanya hadi mapumziko Walimu Fc kuwa kifua mbele.
Kipindi cha Pili kilianza kwa kasi huku Walimu fc wakitaka kuongoza magoli zaidi na Dream Fc kurudisha na kuongeza zaidi.
Alikuwa mshambuliaji hatari wa Dream fc Antony Mtewele aliyefunga goli la kusawazisha na kufanya matokeo kuwa 2- 2 hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa.
Katika mchezo mwingine, Timu ya Nzihi fc walitumia vyema uwanja wao wa nyumbani kwa kuibuka na ushindi wa magoli 2 – 1 dhidi ya Kikongoma Fc katika mchezo uliopigwa katika uwanja wa Kidamali.
Magoli ya Nzihi fc yalifungwa na Allen Mkumbwa na Amasha Mlowosha na goli la kufutia machozi la Kikongoma fc lilifungwa na Dante Mayanga.
Hadi sasa katika mashindano hayo mfungaji bora anayeongoza ni Oscar Evaristo wa timu ya Spana fc aliyefunga magoli matatu katika mchezo mmoja na kukabidhiwa mpira, akifuatiwa na Stephano Malata wa Magulilwa mwenye mabao 2, Antony Mtelewe mwenye mawili.
Michezo mingine itaendelea leo katika viwanja tofauti ambapo Mgama fc watapambana dhidi ya Rangers Fc katika mchezo utakaopigwa kwenye uwanja wa Mgama huku timu ya Luzeni fc watakipiga na Scout fc kwenye uwanja wa Kwakilosa