Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza Ziara ya Kiserikali ya siku 3 katika Jamhuri ya Angola kesho tarehe 07 hadi 09 Aprili, 2025 kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, Mhe. João Manuel Gonçalves Lourenço.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu Sharifa Nyanga imesema Ziara hii inalenga kukuza na kuimarisha zaidi mahusiano ya kihistoria na kidugu kati ya Tanzania na Angola.
Akiwa nchini humo, Rais Dkt. Samia atapata fursa ya kufanya mazungumzo ya uwili na mwenyeji wake Rais Lourenço, kuhutubia Bunge la Angola, kuweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu wa Muasisi wa Taifa hilo Hayati Rais António Agostinho Neto pamoja na kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.
Uhusiano wa Tanzania na Angola uliasisiwa na Waasisi wa mataifa hayo mawili Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Hayati Rais António Agostinho Neto waliokuwa na maono ya pamoja ya kuikomboa Afrika na watu wake.
Uhusiano huu umeendelea kuimarika siku hadi siku na sasa unajikita katika kukuza uchumi hasa katika sekta za biashara, uwekezaji, maendeleo ya miundombinu, mafuta na gesi, madini, uchumi wa buluu, afya, elimu na utalii kama zilivyoainishwa kwenye Tume ya pamoja ya Ushirikiano.
Aidha, ziara hiyo itashuhudia uwekaji saini wa Hati za Makubaliano (MOU) katika masuala yanayolenga kufungua fursa za biashara na uwekezaji na jitihada za kuimarisha ulinzi na usalama.
Pia, Rais Dkt. Samia amealikwa na Spika wa Bunge la Angola, Mhe. Carolina Cerqueira ambae nae pia ni mwanamke, kuhutubia Bunge la nchi hiyo na atakuwa ni Rais wa kwanza Mwanamke kutoka barani Afrika kuhutubia Bunge hilo.
Ikumbukwe kwamba Ziara hii inakuja miaka 19 tangu Maraisi wa Tanzania kufanya ziara za Kiserikali nchini humo ambapo ziara ya kwanza ilifanywa na Baba wa Taifa, ikifuatiwa na Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2006 ambapo pia alihutubia Bunge la nchi hiyo kama Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU).
Rais Dkt. Samia atahitimisha ziara yake kwa kutembelea kiwanda cha mafuta cha Luanda.
Angola ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta na uchumi wake unaendeshwa zaidi na mafuta. Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye hifadhi kubwa ya gesi barani Afrika. Hii inatoa fursa kwa nchi hizi mbili kubadilishana uzoefu katika sekta ya mafuta na gesi pamoja na kujenga uwezo wataalamu wake.