Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Nchini Jenerali Jacob John Mkunda amewapongeza wanamichezo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kufanya vizuri katika michezo mbali mbali ya Kitaifa na Kimataifa kwa kipindi cha robo mwaka kuanzia mwezi Januari hadi Machi 2025 .
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwapongeza wanamichezo hao iliyofanyika katika viunga vya Makao Makuu ya Jeshi Msalato Jijini Dodoma, Jenerali Mkunda amesema mafanikio hayo si ya kawaida kwani yamebeba thamani ya mazoezi, nidhamu, mafunzo, na mshikamano wa Kijeshi, ambapo leo hii wanashuhudia ushindi kutoka michezo ya ngumi, riadha, mpira wa mikono, mpirawa magongo, na mpira wa kikapu.
” Tumeshuhudia medali, vikombe, tuzo, na hata ushindi wa uongozi wa Kimataifa kupitia Meja Mohamed Kasui kwa kuchaguliwa kuwa wa kwanza kutoka Afrika tangu mwaka 1948 kuwa Rais wa Kamati ya Kikapu ya Kijeshi Duniani jambo la kihistoria kwa Tanzania na Afrika”.
Aidha, amesema kuwa Wanajeshi wamekuwa wakilitangaza Jeshi na Nchi Kitaifa na Kimataifa kwa kufanya vizuri katika michezo mbalimbali ambayo wamekuwa wakichaguliwa ama kuteuliwa kushiriki ndani na nje ya nchi.
” Michezo kwetu si burudani tu bali pia ni sehemu ya maandalizi ya Ulinzi wa Taifa, na hili ningependa iwe sehemu ya wajibu wa timu hizi au walezi wa michezo niliowateua “.
Naye Mkuu wa Operesheni na Utendaji Kivita Jeshini Meja Jenerali Ibrahim Mhona amesema kuwa wanamichezo wote waliofanikiwa wameonesha kuwa Askari wa JWTZ wanaweza kuwa shujaa ndani ya Uwanja wa Vita na Uwanja wa Michezo.
Wanamichezo waliofanya vizuri kimataifa ni pamoja na Praiveti King Lucas Mwajobaga ambaye ni Bingwa wa ngumi uzito wa Bantam Weight Afrika baada ya kumbwaga bingwa wa Angola yaliyofanyika Nchini Tunisia, Februari 2025.
Kwa upande wa mbio za Nyika timu ya wanaume waliibuka washindi wa kwanza katika mashindano ya Majeshi ya Dunia kipindi cha baridi (CISM Winter Games) Nchini Uswisi.
Timu ya Wanawake mbio za Nyika walishika nafasi ya tatu Machi 2025, huku praiveti Joseph Panga akishika nafasi ya pili kati ya wakimbiaji wa Mataifa zaidi ya 40.
Hafla hii ni kielelezo cha jinsi ambavyo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda anathamini nafasi ya michezo katika ujenzi wa Jeshi thabiti, lenye mshikamano na heshima.