…………..
Na Sabiha Khamis Maelezo
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mhe. Ali Suleiman Ameir amewataka wananchi kudumisha uzalendo ambao viongozi na waasisi wa Mapinduzi wameuanzisha ili kusaidia kuleta maendeleo nchini.
“Nchi hii haitofanikiwa, haito lindwa, haitokwenda mbele pasipo kuwa na uzalendo hawa wazee wetu waliweka uzalendo mbele ili kufanikiwa” alisema Mhe. Suleiman.
Ametoa wito huo katika ziara ya kusoma dua kaburi la Marehemu Mohamed Abdallah Kaujore, Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharib B Unguja, amesema Marehemu Mohamed ni miongoni mwa waasisi waliyoikomboa nchi kwa kujitolea muhanga ili kuhakikisha nchi inapata uhuru wake.
Amesema uzalendo unapodumishwa katika nchi huwa kinga ya maendeleo ambayo itasaidia kuendelea kuwaenzi na kuwathamini viongozi waliopita kwa mazuri ambayo wameyafanya na kuyaacha na viongozi hao kwa maendeleo ya nchi na vizazi vijavyo.
Hata hivyo amesisitiza amani na utulivu katika nchi kwa kuthamini mazuri na juhudi walizozifanya viongozi na waasisi wa Mapinduzi kwa kuyatunza na kuyaendeleza mema na mazuri yao kwa kudumisha umoja na mshikamano.
Akizungumza kwa niaba ya familia Mjukuu wa Marehemu Ndugu Mohamed Abdalla amesema wanaishukuru Serikali kwa kujumuika na familia hiyo na kuweka utaratibu wa kuwaombea dua viongozi na waasisi wa Mapinduzi jambo ambalo huleta umoja na mshikamano kwa kuifanya familia kuona bado Serikali inaendelea kuwathamini viongozi na waasisi hao.
Maadhimisho ya wiki ya kuwaenzi viongozi wa Kitaifa, Waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar na Katibu wa kwanza wa Chama cha Afro Shirazi ambapo kilele kitafanyika Aprili 7, 2025 Kisiwandui Wilaya ya Mjini, Unguja.