Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Bw. Mathias Cormann, Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo Jijini Paris nchini Ufaransa, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana namna Tanzania na Shirika hilo wanavyoweza kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa sera za kodi, usimamizi wa fedha za umma, mageuzi ya taasisi za kifedha na kuimarisha masuala ya uwekezaji nchini Tanzania.




(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha-Paris)
………….
Na Benny Mwaipaja, WF, Paris Ufaransa
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Bw. Mathias Cormann, Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo Jijini Paris nchini Ufaransa, ambapo pamoja na mambo mengine wamejadiliana namna Tanzania na Shirika hilo wanavyoweza kushirikiana katika kuimarisha usimamizi wa sera za kodi, usimamizi wa fedha za umma, mageuzi ya taasisi za kifedha na kuimarisha masuala ya uwekezaji nchini Tanzania.
Mhe. Dkt. Nchemba ilieleza dhamira ya Serikali ya kuimarisha uwezo wa taasisi zake za kifedha kwa kupokea usaidizi wa kitaalamu kutoka OECD katika maeneo hayo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza mapato ya ndani, kuvutia uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Shirika hilo kwa kupokea utaalam katika kuimarisha vyanzo vya mapato ya ndani, kuimarisha uwekezaji na kukuza uchumi jumuishi utakaochangia kuimarisha mapato yake ya ndani, kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara na hatimaye kukuza uchumi na maendeleo ya wananchi kwa ujumla.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania inakubaliana na utozaji wa kodi wenye usawa katika uwekezaji hususani katika uchumi wa kidigitali hivyo Tanzania inaendelea kuliomba Shirika la OECD kutoa mafunzo ya kiufundi katika eneo hilo.
“Tanzania itaweza kuimarisha usimamizi wa fedha za umma, kuongeza uwazi, na kuvutia mitaji ya kimataifa inayohitajika kwa utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030” alisema Mhe. Dkt. Nchemba.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Bw. Mathias Cormann alisema kuwa Shirika lake liko tayari kushirikiana na Tanzania katika masuala ya usimamizi wa sera za kodi na uwekezaji ili kukuza Uchumi wa nchi kwa kuvutia zaidi mitaji kutoka nje ya nchi.
Ameipongeza Tanzania kwa juhudi zake katika kuhakikisha kunakuwa na kodi zenye usawa hususani katika mazingira yaliyopo sasa ya uchumi wa kidigitali na kuishauri walishauri Tanzania ijiunge na Kituo cha Maendeleo cha OECD, ambacho kwa sasa kina nchi wanachama 12 kutoka Afrika.
Bw. Cormann alizitaja faida za kuwa mwanachama wa kituo hicho ni pamoja na kuchapishwa kwa takwimu za mapato ya kodi (Revenue Statistics), ambazo hutoa uwazi kwa wawekezaji na wadau wa maendeleo, na kusaidia nchi kuonyesha uwezo wake wa kifedha kwa taasisi za fedha za kimataifa na wawekezaji binafsi.
Aidha, aliialika Tanzania kushiriki katika Mkutano wa Jukwaa la Misaada kwa Maendeleo Endelevu, utakaofanyika mwezi Mei mwaka huu, mkutano ambao utatoa nafasi kwa Tanzania kuwasilisha vipaumbele vyake vya maendeleo, kujifunza kutoka kwa wengine, na kuanzisha ushirikiano mpya katika sekta za mazingira, mabadiliko ya tabianchi na uchumi jumuishi.