Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea na juhudi za kuboresha sekta ya usafiri wa reli kwa kuanzisha mradi wa Reli ya Jiji la Dar es Salaam (Commuter Rail Network – CRN).
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, amesema mradi huu utaimarisha mfumo wa usafiri wa umma kwa kuwapa wakazi wa Dar es Salaam njia mbadala na ya uhakika ya kusafiri.
Akizungumza katika kikao kazi na wanahabari wa mitandao ya kijamii kilichofanyika Morogoro, Kadogosa amesema kuwa CRN itasaidia kupunguza msongamano wa magari barabarani huku ikirahisisha safari za kila siku kwa maelfu ya wakazi wa jiji.
“Ujenzi wa reli ya jiji la Dar es Salaam ni jambo la lazima. Tunaweka mkazo katika kuboresha miundombinu ya usafiri wa reli ili kuongeza ufanisi kwa wananchi,” alisema Kadogosa.
Kwa mujibu wa TRC, mradi huo utahusisha treni za kisasa zitakazorahisisha usafiri wa abiria kutoka maeneo ya pembezoni kwenda katikati ya jiji na maeneo mengine muhimu kama vituo vya biashara, shule, vituo vya afya, na sehemu za kazi.
Kadogosa alifafanua kuwa usanifu wa awali na upembuzi yakinifu wa reli hiyo umekamilika, huku taratibu za utafutaji wa fedha zikiendelea ili kuanza utekelezaji wake mapema. Pia, reli ya Dodoma ipo katika hatua hiyo na utekelezaji wake unatarajiwa kuanza kabla ya Dar es Salaam, kisha kufuatiwa na Arusha na Mbeya.
Kwa upande wa ushirikiano wa sekta binafsi, Kadogosa alieleza kuwa kampuni kadhaa zimeonesha nia ya kushiriki katika ujenzi wa reli hiyo, ikiwemo kampuni ya Alstom.
Mradi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa TRC wa kuendeleza miundombinu ya reli nchini, ukienda sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR). Kadogosa aliipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika miradi ya SGR, akibainisha kuwa thamani ya mikataba iliyosainiwa hadi sasa ni takribani shilingi trilioni 29.58.
Mbali na maendeleo ya ndani, Tanzania kupitia TRC pia imepewa heshima ya kutoa mafunzo kwa wataalamu wa reli kutoka Burundi, ikiwa ni ishara ya kuaminika kwa nchi jirani katika sekta ya reli.
Kupitia miradi hii, Tanzania inajidhatiti kuwa kitovu cha usafiri wa reli barani Afrika, ikihakikisha kuwa wananchi wake wanapata huduma bora za usafiri wa kisasa na wa gharama nafuu.