WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff (kulia), akivuta kitambaa kuzindua Jumuiya ya Wawekezaji wa Nyumba za Biashara (REDA), hafla iliofanyika hoteli ya Golden Tulip Uwanja Ndege Zanzibar. Kushoto ni Mwenyekiti wa REDA Marcin Fillipczyk
…………………
NA MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Shariff Ali Shariff, amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeonesha azma ya kuiunga mkono Jumuiya ya Wawekezaji wa Nyumba za Biashara (REDA) kama njia muhimu ya kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jumuiya hiyo katika Hoteli ya Golden Tulip, Zanzibar, Waziri Shariff alisisitiza kuwa uwekezaji katika sekta hiyo utachangia maendeleo ya uchumi wa Zanzibar na kuleta manufaa kwa wananchi kupitia mikakati ya serikali. Alieleza kuwa REDA inaendana na malengo ya serikali kwa kusaidia Zanzibar kupiga hatua katika ramani ya dunia kwa kuimarisha sekta ya nyumba za biashara.
“Serikali itaendelea kutoa msukumo ili wawekezaji wa sekta hii wafikie malengo yao, na kwa pamoja tuweze kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini,” alisema Shariff.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa REDA, Marcin Fillipczyk, alisema kuwa jumuiya hiyo inalenga kuwaunganisha wawekezaji wa ardhi kutoka pande zote za nchi na kuwapa nafasi ya kushirikiana, kubadilishana uzoefu, na kushughulikia changamoto zinazowakabili. Alisisitiza umuhimu wa kuunda sera bora zitakazowezesha ujenzi wa nyumba za bei nafuu kwa wananchi wa kipato cha chini.
Aliongeza kuwa ushirikiano na serikali ni muhimu ili kutatua changamoto za upatikanaji wa ardhi, urasimu wa kupata vibali, na matatizo ya kifedha yanayowakabili wawekezaji wa sekta hiyo.
Naye Mwanasheria wa jumuiya hiyo, Masoud Salim Mohammed, alielezea kuwa REDA inakusudia kuwa na sauti moja kwa wawekezaji ili kutoa ushauri kwa serikali na kuhakikisha kuwa kuna sheria rafiki kwa maendeleo ya sekta ya uwekezaji. Alibainisha kuwa kwa kushirikiana na serikali, wawekezaji wataweza kutoa mapendekezo na ushauri kuhusu masuala ya maendeleo.
Aidha, aliwataka Wazanzibari kutumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta ya nyumba za biashara na kuhakikisha wanapata mafunzo ya kitaalamu ili kuepuka kufanya kazi kimazoea.
Jumuiya hiyo, ambayo ilisajiliwa rasmi mwaka 2023, kwa sasa inajumuisha wanachama 10 kutoka nchi mbalimbali. Uungaji mkono wa serikali kwa juhudi za REDA ni ishara ya kuimarika kwa sekta ya uwekezaji na uchumi wa Zanzibar, ikiwa ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya taifa.