Akizungumza na waandishi wa habari Jijini, Dar es Salaam tarehe 03 Aprili, 2025 Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amesema kuwa wameingia makubaliano hayo kwa sababu taasisi hizo zinashabihiana kwenye suala la ujenzi na hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati.
Amesema kupitia makubaliano hayo wanatarajia kuboresha zaidi kwa ujuzi na umahiri wao katika mikataba ya ujenzi.
*“Tumeshuhudia Serikali ya Awamu ya Sita ikiendelea na jitihada zake za kufanya miradi mikubwa na ya kimkakati ya ujenzi, kwa hiyo sisi kama wanasheria, wataalamu wa ujenzi tunatakiwa kuhakikisha kwamba tunakuwa na ujuzi na utaalamu stahiki kuhakikisha miradi hii ya ujenzi mikubwa inafanyika vizuri na mikataba inaandaliwa na kutekelezwa vizuri, pia usimamizi wake unakuwa mzuri,”* amesema Mhe. Johari
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa wataalamu wa ujenzi kutoka Baraza la Taifa la Ujenzi na wanasheria kwa upande wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lazima wafanye kazi kama timu kama kweli wanataka kuhakikisha mikataba ya ujenzi na taaluma yake inafanyika vizuri.
*“Ni jambo ambalo tunaamini tukilifanya tukiwa na hati hii ya makubaliano tutaweza kubadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo wataalamu wetu watafahamu masuala haya yanayohusiana na sekta ya ujenzi kwa kina zaidi.* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Vilevile Mhe. Johari ameendelea kueleza kuwa anataka wabadilishane utaalamu kwa kupata ushauri wa kitaalamu katika masuala yote yanayohusu sekta ya ujenzi.
*“Lakini pili nilizungumza kwenye mafunzo yetu kule Arusha kwamba mafunzo tunakwenda kuyapa kipaumbele kikubwa sana, na mafunzo yapo ya aina mbalimbali mojawapo ni kubadilishana kama hivi kwa kushirikiana na taasisi nyingine ambao wao wana ubobezi kwenye eneo fulani, tunabadilishana wataalamu na kwa kufanya hivyo unajikuta wataalamu wako wanapata mafunzo stahiki kwa maana wa pande zote mbili Baraza la Taifa la Ujenzi wanapata mafunzo ya kile tunachofanya na sisi tunapata uzoefu wa kile wanachofanya.* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameelezea kuwa, Ofisi hizo zinahitaji kushirikiana katika kufanya uchambuzi wa madai yatokanayo na mikataba ya ujenzi na suala la majadiliano ya mikataba ya ujenzi.
*“Kwa sababu mikataba ya ujenzi iko tofauti kidogo na mikataba ya huduma,tukae pamoja tuone ni vitu gani tunapaswa kuvizingatia katika mikataba ya ujenzi ili kuhakikisha mkataba huo unakaa vizuri sababu wakati wa utekelezaji wake unaweza kujikuta unakwama kumbe kwenye majadiliano haukuzingatia vitu muhimu matokeo yake ukazaa mkataba ambao hauna vile vitu vya msingi ambavyo Baraza la Taifa la Ujenzi linavifahamu na linasisitiza vizingatiwe katika mikataba ya ujenzi.* ameeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Sambamba na hilo Mhe Johari amesema ni muhimu kwa wataalamu kutoka katika Ofisi yake wakaelewa kwa kina masuala ya sekta ya ujenzi kutokana na upekee wake hivyo kuwasaidia katika usuluhishi wa migogoro na mikataba ya ujenzi.
*”Mikataba ya ujenzi yenyewe ina upekee wake ambao sisi tunaamini ni muhimu sana tukaifahamu pamoja masuala mengine mtambuka yanayozingatia sekta ya ujenzi nchini na mambo mengine katika sekta ya sheria ili tushirikiane vizuri”.* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi, Bw. Matiko Mturi amesema makubaliano hayo ni fursa kubwa kwao katika kujifunza na kuchota ujuzi wa kisheria kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
*“Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ndiyo inayosimamia na kuhakikisha mikataba yote ya Tanzania iko vizuri na mojawapo ni mikataba ya sekta ya ujenzi kama mnavyojua sasa hivi kuna mikataba mingi ya miradi mikubwa kwa hiyo lilipokuja wazo la kushirikiana tuliona linaoana kabisa na azma yetu ya kuhakikisha miradi ya sekta ya ujenzi inatekelezwa vizuri.”* Amesema Bw. Matiko
Katika hatua nyingine, Bw. Matiko amesema tangu kuanzishwa kwa Baraza hilo mnamo mwaka 1981 wametekeleza masuala mbalimbali ya ujenzi na wanafahamu vipengele vingi ambavyo huwa vina changamoto hivyo lilipokuja suala la kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu waliona ni nafasi nzuri kwao.